Sunday, 30 November 2014
MKULIMA APIGWA RISASI NA POLISI BAADA YA KUVAMIA KITUO HUKO SINGIDA
MKULIMA mkazi wa kijiji cha Mitundu tarafa ya Itigi wilaya ya Manyoni mkoa wa Singida,Esther Salumba (30) amefariki dunia baada ya kupigwa risasi na polisi wakati wa vurugu za kuvamia kituo kidogo cha polisi kilichopo kijijini hapo.
Esther alipigwa risasi kwenye paja na mguu wa kulia ambapo alivunja damu nyingi na zilizopelekea kifo chake papo hapo.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, ACP Thobias Sedoyeka, alisema tukio hilo limetokea Novemba 26 mwaka huu saa 7.30 mchana huko katika kijiji cha Mitundu.
Alisema siku ya tukio askari polisi wa kituo kidogo cha Mitundu, walimkamata Tisho Simon (28) kwa tuhuma ya kutenda kosa la jinai.
Sedoyeka alisema wakati mtuhumiwa anawekwa mahabusu, mtuhumiwa huyo alianza kufanya vurugu huku akigoma kuinuia mahabusu.
“Kutokana na mvutano kati ya Tisho na askari,Tisho alijigonga ukutani na kuumia.Ndugu zake walipata taarifa na kukusanyanya pamoja na majirani na kuvamia kituo cha polisi wakiwa wamebeba silaha za jadi na galoni ya lita tano iliyokuwa na petroli lengo likiwa ni kukiteketeza kituo chetu”,alisema Sedoyeka.
Alisema askari polisi walijitahidi kuwatawanya wananchi hao kwa njia za amani,lakini juhudi hizo ziligonga mwamba,na wananchi hao waliendelea kurusha mawe na kuanza kubomoa ukuta,kitendo kilichopelekea askari kurusha risasi ya moto hewani kwa lengo la kuwatawanya.
“Katika purukushani hizo,wananchi wanne walijeruhiwa na kati yao watatu walijeruhiwa kwa risasi na mmoja alishambuliwa na wananchi kwa tuhuma ya kusaidia askari polisi”,alisema kamanda huyo.
Sedoyeka alitaja waliojeruhiwa kwa risasi kuwa ni Jonas Rubein (29) na Mohammed Madole.Simon Christian (22),alijeruhiwa na wananchi waliokuwa wakimtuhumu kuwasaidia askari polisi.
Katika hatua nyingine, kamanda Sedoyeka, alisema baadhi ya viongozi na Mtemi wa eneo hilo la Mitundu,wameliomba radhi jeshi la polisi kwa tukio hilo na wamelisihi lisiondoe kituo hicho kijijini hapo.
Alisema viongozi hao na baadhi ya wananchi,wameweza kukikarabati kituo hicho pamoja na kununua mabati na matofali ili kukirudisha kituo kwenye hali yake ya kawaida.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment