Saturday 6 December 2014

JELA KWELI KUBAYA...KENYATTA AFURAHIA KUACHIWA HURU


RAIS Uhuru Kenyatta ameelezea kufurahishwa na uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), kutupilia mbali kesi ya jinai iliyokuwa ikimkabili, baada ya Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Mahakama hiyo, Fatou Bensouda kuondoa mashitaka dhidi ya Rais huyo.



Bensouda alisema katika taarifa yake jana kuwa, hawezi kuendelea na mashitaka dhidi ya Rais Kenyatta, baada ya Jumatano wiki hii Majaji wa Mahakama hiyo, kumpa wiki moja kuja na ushahidi wa kutosha wa kuendelea na kesi hiyo.

Baada ya kupata taarifa hiyo, Rais Kenyatta alisema yeye na familia yake wamefurahishwa na taarifa hizo na kutania kuwa, mkewe angekuwepo karibu, angemkumbatia kwa furaha.

“Angekuwa karibu, ningemkumbatia na kumshukuru kwa ushirikiano na mawazo ya kunitia moyo aliyonipa,” alisema. Aidha katika akaunti yake ya Twitter, Kenyatta aliandika; ”Nimepokea habari kwamba kiongozi wa mashitaka ICC ametupilia mbali kesi dhidi yangu.

Daima nimekuwa nikisema kuwa kesi za Kenya ziliharakishwa sana kupelekwa ICC bila kufanyiwa uchunguzi wa kina. “Mara kwa mara nimekuwa nikiwasisitizia Wakenya na dunia nzima kuwa sina hatia, uamuzi huu ni afueni kubwa sana kwangu kwani ulipaswa kutolewa miaka sita iliyopita.

“Nimefurahishwa sana na habari hizi ambazo nimekuwa nikizisubiri tangu jina langu lihusishwe na kesi iliyowasilishwa Hague dhidi yangu,” alisema.

Kenyatta alishtakiwa kama Mshitakiwa Mkuu wa ghasia zilizoibuka baada ya uchaguzi wa mwaka 2007/2008, akidaiwa pamoja na William Ruto ambaye ni Naibu Rais, kutenda uhalifu dhidi ya binadamu.

Mbali na mashitaka hayo, Kenyatta ameweka rekodi ya kuwa Rais wa Kwanza aliyeko madarakani kufikishwa mbele ya Mahakama hiyo, baada ya kufunguliwa mashitaka mwaka 2012.

Hili ni pigo kubwa kwa upande wa mashitaka, kwani wengi waliiona kesi dhidi ya Kenyatta kama mtihani mkubwa katika historia ya Mahakama hiyo.

Upande wa mashitaka ulitaka Mahakama kuipatia muda zaidi ili utafute ushahidi zaidi dhidi ya Kenyatta kama vile taarifa za akaunti yake ya benki. Hata hivyo upande wa utetezi ulitoa utetezi wake kuwa iwapo hakuna ushahidi wa kutosha, kesi hiyo inapaswa kufutwa.

Naibu Rais Ruto naye ameshitakiwa kwa tuhuma kama hizo ICC, baada ya juhudi za wanasheria wake kutaka mteja wao afutiwe kesi.

Ruto na Kenyatta walikuwa pande pinzani wakati wa uchaguzi wa mwaka 2007, huku Ruto akituhumiwa kuchochea vurugu ili kuzuia kiongozi wa upinzani Raila Odinga nafasi ya kuwa Rais.

Hata hivyo alikanusha kuhusika na tuhuma hizo. Ruto aliungana na Kenyatta katika uchaguzi wa mwaka 2013, na kumfungulia njia ya kuwa Naibu Rais.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema Kenyatta kufutiwa kesi wakati kesi ya Ruto bado inaendelea kunaweza kuleta mgogoro wa kisiasa na kuibua hali tete ya masuala ya ukabila nchini humo.

No comments: