Monday 1 December 2014

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI ASISITIZA FEDHA ZA ESCROW SI ZA SERIKALI


Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema ameomba uamuzi wa wabunge utakaotolewa usiathiri kesi zilizopo mahakamani kuhusiana na mgogoro wa IPTL/ Escrow.
   

Akichangia katika mjadala wa ripoti ya PAC ambayo ilimtaka pia ajiuzulu, Werema alisema analazimika kutoa ufafanuzi wa baadhi ya maeneo ya ripoti hiyo kwa kuwa anaona kuna maeneo mengi ambayo yamepotoshwa na hakubaliani nayo.
"Hadi sasa mimi msimamo wangu ni kwamba taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na ndivyo ilivyo haukuthibitisha popote kwamba fedha hizi ni za Serikali. Japokuwa alieleza kwamba katika fedha hizo upo uwezekano wa kuwapo fedha za Serikali," alisema.
Alieleza kwamba taarifa hiyo ya CAG iliziondoa Sh167 bilioni katika tarifa yake, akisema kuwa kuwa siyo fedha za Serikali na kwamba aliainisha katika ukurasa wa 52 kwamba hiyo siyo fedha ya umma.

Werema alisema alishaiomba mahakama kuharakisha kesi zote zinazohusiana na mgogoro huo ili zimalizike kabla ya Sikukuu ya Krismasi mwaka huu, huku akiwaomba msamaha majaji wanaoshughulikia kesi hizo, bila kutoa ufafanuzi wa msamaha huo.
Hata hivyo, alieleza kwamba msingi wa makubaliano kwenye mkutano uliofanyika Hoteli ya Kunduchi jijini Dar es Salaam na kutoa uamuzi wa fedha hizo kutolewa Benki Kuu na kulipwa kwa wahusika, ulikuwa sahihi kwa kuwa ulifanyika baada ya pande zote kuafikiana.
Akihitimisha kwa upole, Jaji Werema ambaye amekuwa akisimama kidete kutetea hoja zake kwa ujasiri, alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa yote yanayoendelea, kisha alikaa chini baada ya muda wake kumalizika.
Chanzo:Mwananchi

No comments: