Friday 5 December 2014

BINTI AOLEWA KWA KILO MBILI TU ZA SUKARI


Mmoja wa wanafunzi walioongoza mtihani wa Taifa wa Darasa la saba mwaka huu mwenye umri wa miaka 16 anadaiwa kuozwa kwa mwanaume mwenye miaka 50 baada ya wazazi wake kupewa sukari kilo mbili kama mahari.Kutokana na hali hiyo mtandao wa kuelimisha jamii kuhusu ukeketeji Mkoani Kilimanjaro NAFGEM umefanya jitihada za kumuokoa pamoja na wanafunzi wengine15 waliotaka kufanyiwa vitendo vya ukeketaji kwa ngariba.


Msichana huyo wa miaka 16 wa kabila la kimasai ambaye jina lake limehifadhiwa baada ya kufaulu mtihani huo kwa asilimia kubwa huku akitajwa kuwa miongoni mwa wasichana waliofanya vizuri aliozeshwa kwa mwanaume mmoja ambaye ni mfugaji wa kabila hilo. 

Meneja Mpango wa mtandao wa kuelimisha jamii kuhusu ukeketaji Mkoani Kilimanjaro Honoratha Nasua alitoa taarifa za kuolewa kwa binti huyo walizipatahuku wanafunzi wengine 15 wakisubiri tarehe ya kufanyiwa ukeketaji ili waozeshwe baada ya tendo hilo. 

Alisema suala la mwanafunzi huyo aliyeozeshwa limefikishwa katika dawati la jinsia la Polisi Wilayani Siha kwa ajili ya kuchukua hatua zaidi za kisheria. 

Alisema wazazi wa mwanafunzi huyo wamechangia kudidimiza maendeleo ya mtoto wao kwa kukubali aolewe na kubuni mbinu mpya ya kukeketa watoto wachanga ili kukwepa mkono wa dola na vyombo vya wanaharakati. 

Mtandao huo wa kupinga ukeketaji unaendelea na shughuli zake katika Wilaya hiyo ikishirikiana na Shirika la kimataifa la Elimu kwa ufadhili wa Shirika la misaada la kimataifa la Marekani USAID kupitia mpango wa pamoja wa TUWALEE!
Chanzo: Nipashe

No comments: