Tuesday 2 December 2014

VIRUSI VYA UKIMWI VYAPUNGUA NGUVU......


Utafiti mkubwa wa kisayansi umeonyesha kuwa virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi vya HIV, vinapungua makali yake na kushuka kwa uwezo wake wa maambukizi kwa jinsi vinavyobadilika. Watafiti katika chuo kikuu cha Oxford nchini Uingereza wamefanya ugunduzi huo walipowafanyia uchunguzi mamia ya wanawake nchini Botswana.    
 


Kikosi hicho cha madaktari kimegundua kuwa virusi vya HIV vilikuwa vikiingia katika hatua ya kuharibu mabadiliko yake ili kuishi na kwa kufanya hivyo, virusi hivyo kwa sasa vinabadilika taratibu zaidi na inavichukua muda mrefu zaidi kusababisha ugonjwa wa UKIMWI kwa watu wenye kuishi na virusi hivyo. Wanasayansi hao wamesema kupungua kwa makali ya virusi vya HIV kutaweza kusaidia jitihada za kutokomeza virusi hivyo, japokuwa wameonya kuwa virusi hivyo dhaifu bado ni hatari kwa afya ya binadamu.

                                                Virusi vya Ukimwi katika muonekano tofauti.  
Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Ukimwi Duniani, Desemba Mosi ya kila mwaka, takwimu zinaonyesha juhudi zilizofanyika katika kupambana na ugonjwa huo.
Maambukizi ya virusi vya Ukimwi yameshuka kwa asilimia 38 tangu mwaka 2001 na idadi ya vifo vinavyotokana na ugonjwa wa Ukimwi vimepungua kutoka zaidi ya milioni 2.3 mwaka 2005 hadi milioni 1.5 mwaka 2013.
Haya yakiwa maendeleo mazuri, bado idadi kubwa ya watu wapatao milioni 35 wanaishi na virusi vya Ukimwi. Kila siku zaidi ya watu 5,700 wanaambukizwa virusi vya Ukimwi, sawa na watu karibu 240 kila saa.

Ifikapo mwaka 2015, watoto milioni 25 watapoteza mzazi mmoja au wote wawili kutokana na ugonjwa wa UKIMWI.
Ugonjwa huu ni janga kubwa la kijamii duniani.UKIWMI si tu unawanyang'anya mamilioni ya watoto maskini kabisa, upendo na ulinzi kutoka kwa wazazi wao, bali pia watoto wengiwanabakia kuhangaika peke yao, wengi wakiwa na jukumu la kuwalea wadogo zao, katika hali ya umaskini mkubwa, kubaguliwa na unyanyapaa unaosababishwa na maambukizi ya virusi vya HIV. Watoto wengi wanatengwa na mara nyingi ndugu wa familia zao hawawezi kuwatunza.
CHANZO:BBC

No comments: