Saturday, 6 December 2014

JINSI UKIMWI ULIVYOANZA AFRIKA


Ulianzia Jamhuri ya Demkorasia ya Congo (DRC) na vitendo vya ngono kwenye vituo na safari za treni mjini Kinshasa vilichochea ugonjwa huo kuanza kuenea kwa kasi hadi nje ya mipaka ya nchi hiyo.



Wakati ugonjwa wa ukimwi ukipamba moto katika mataifa mengi ya Afrika, miaka ya 1980, ilizuka hofu kubwa na maswali mengi juu ya lilikoanzia.

Kwa mfano, hapa Tanzania ulipewa majina mengi, kama vile Juliana, silimu (wembamba), fire (moto) na mdudu. Ni ugonjwa ambao walioupata walionekana kukonda hadi kubakia mifupa na nywele kunyonyoka.

Mbali na hali hiyo, mgonjwa alipata matatizo ya ngozi kuharibika kwa kuwa kavu, vidonda ambavyo viliacha madoa meusi na kuharisha.

Sura za wagonjwa zilikuwa zinabadilika na kuonekana za kutisha na walionekana kuwa katika hali ya mateso mengi ya kukumbwa na maradhi mengi kabla ya kufa.

Inafahamika wazi kuwa binadamu lazima utafika wakati atakufa, lakini kwenye miaka ya 1980 hadi mwanzoni mwa 1990, ulionekana kuambkizwa Virusi Vya Ukimwi (VVU) ni sawa na kupewa tiketi ya kifo. Wengine walidiriki hata kujiua mara baada ya kubaini wameambukizwa.

VVU inaweza kuchukua miaka mitano hadi zaidi ya 10 ili kuonyesha dalili za kuugua, hatua ambayo inafahamika kuwa ni ya ukimwi.

Wengi wa waliopimwa na kuonekana wameambukizwa wakati huo walifika hatua ya kukonda na kuugua mapema kutokana na wasiwasi na msongo wa mawazo juu ya kifo.

Zipo dhana nyingi katika jamii zinazohusu jinsi Viruzi Vya Ukimwi (VVU) vilivyoanza kuenea kwa binadamu, hususani kwa Waafrika ambao ndio wanaonekana kuathirika zaidi na janga hili.

Zilikuwapo dhana nyingi sana na zote zimefanyiwa kazi na wataalamu wa afya. Baada ya uchunguzi wa kina dhana nne ndizo zilizofanyiwa utafiti wa kina baada kuonekana kuwa mojawapo inaweza ikawa ni chanzo.

Dhana zilizofanyiwa kazi ni nne nazo ni za madai ya hujuma zilizofanywa na wataalamu ili kuwaua Waafrika, ukatili wa kikoloni, matumizi ya chanjo na shughuli za uwindaji.
Hii ilitokana na hisia za Waafrika wenyewe hasa ikizingatiwa kuwa wao ndio waliokuwa wanaathirika zaidi.
Chanzo: Mwananchi

No comments: