Wednesday, 3 December 2014

HATARI!!!!!! WAGONJWA WAUWANA WODINI JIJINI ARUSHA




Mgonjwa Hashimu Mohammed Mollel (28) anayetuhumiwa kumuua mgonjwa mwenzake, Lazaro Mollel (75) aliyelazwa naye katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru,Arusha.
MAAJABU! Katika hali isiyo ya kawaida mgonjwa aliyelazwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru, akisumbuliwa na maradhi ya mguu, Hashimu Mohammed Mollel (28), (pichani) mkazi wa Lemala, Arusha amemuua mgonjwa mwenzake aliyelazwa naye, Lazaro Mollel (75) kwa kumpiga na chuma cha kutundikia dripu.
Tukio hilo la aina yake lilitokea Novemba 22, mwaka huu saa 6 usiku katika wodi ya majeruhi baada ya mtuhumiwa huyo kuzua tafrani kwa kutaka kupiga wenzake, hali iliyosababisha wagonjwa mbalimbali kutimua mbio na kujificha kuokoa maisha yao na kumuacha marehemu ambaye alikuwa hajiwezi akiwa amelala kitandani. 

Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo walieleza kuwa, Hashimu ambaye bado amelazwa katika wodi hiyo akiwa amefungwa pingu mkononi, chini ya ulinzi wa polisi, alieleza kuwa mnamo muda huo mtuhumiwa alitenda kosa hilo baada ya kumaliza kuswali. 
‘’Kabla ya kuanza swala mtuhumiwa huyo alimuomba kijana aliyekuwa akimuuguza ampeleke kujisaidia,” alisema shuhuda huyo ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini.Aliongeza kuwa baada ya kurejea alipiga magoti na kuanza kuswali chini ya kitanda alichokuwa amelazwa na baadaye alipomaliza aliwaamuru wagonjwa wenzake wazime taa.
“Baada ya taa hizo za wodini kuzimwa mtuhumiwa alisikika
akisema kwa sauti kubwa kuwa leo anataka kuua mtu huku akivurugavuruga vitu kwenye vitanda vya wagonjwa kikiwemo cha kwake na kupiga kelele kwa sauti kubwa, hali iliyowafanya wagonjwa wengine kutimua mbio. Hata hivyo, wakati vurugu hizo zikiendelea muuguzi wa zamu alitoa taarifa kwa kupiga simu kituo cha polisi mjini kati. 

Wakati askari polisi wakisubiriwa mtuhumiwa aliendelea na vurugu na kuchukua chuma cha kutundikia drip na kuivunja kisha kwenda kumpiga kichwani marehemu aliyekuwa amelala pekee kwenye wodi hiyo akiuguza mguu wake wa kulia na alifariki dunia papo hapo. 

Polisi walipofika walikuta ameshaua na alikamatwa na kuchomwa sindano ya dawa ya usingizi, ndipo akadhibitiwa.Mganga mkuu wa hospitali hiyo, Josian Mlay alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa mtuhumiwa huyo hakuwa na matatizo yoyote ya akili. Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, SACP Liberatus Sabas alikiri kutokea kwa tukio hilo.

No comments: