Wednesday 3 December 2014

SPIKA: MSIOE WANAWAKE WALIOKEKETWA...


Spika wa Bunge la Uganda Bi Rebecca Kadaga amewashauri wanaume kutowaoa wanawake waliokeketwa akiwataja kuwa mzigo ambao hauwezi kuijenga jamii.


Kulingana na gazeti la daily Monitor,Spika Kadaga alitoa wito huo wakati wa sherehe ya kitamaduni ambayo inapinga ukeketaji ilioandaliwa na mfuko wa umoja wa mataifa unaosimamia idadi ya watu na wahisani wengine.

''Mwanamke ambaye amekeketwa hana thamani yoyote. Achaneni na wanawake waliokwenda kukeketwa na badala yake chagueni wanawake ambao hawakukeketwa na ambao wanaweza kuimarisha jamii'',alisema Bi Kadaga.

Utamaduni huo unaojulikana kama upashaji tohara wanawake umekithiri miongoni mwa tamaduni nyingi na bara la Afrika kwa jumla na hutumiwa kumuandaa mwanamke anayeolewa ama hata kuonyesha kwamba ,mwanamke amebalehe.

Nchini Uganda ,utamaduni huo hufanyika mashariki mwa Uganda katika makabila matatu ikiwemo lile la Pokot,Sabiny na Tepeth hususan katika wilaya za Kampchorwa,Kween na Bukwo.

Bi Kadaga ambaye aliyeandamana na waziri wa maswala ya kijinsia Rukia Nakadama wote walitia sahihi ya kumaliza ukeketaji nchini Uganda.

Pia aliwaonya wazazi katika eneo hilo kukoma kuwalazimisha wanao katika ndoa za mapema na badala yake kuwataka kuwapeleka shule.

Baadhi ya wanawake waliokuwa wakitekeleza tendo hilo waliiomba serikali kulisaidia kundi la watu ambao wamewacha kuwapasha tohara wanawake.

No comments: