Saturday, 6 December 2014

MMAREKANI MWEUSI MWINGINE APIGWA RISASI..


Mmarekani mwingine mweusi ambaye hakuwa na silaha ya aina yoyote ameuawa kwa kupigwa risasi na polisi mzungu huku maelfu ya Wamarekani wakiendelea kufanya maandamano kupinga mauaji ya kibaguzi yanayowalenga Wamarekani wenye asili ya Afrika. 


Afisa wa polisi wa mji wa Phoenix katika jimbo la Arizona amempiga risasi na kumuua Rumain Brisbon aliyekuwa na umri wa miaka 34. Idara ya Polisi ya mji wa Phoenix imetoa taarifa haraka ikidai kuwa afisa huyo wa polisi aliambiwa kuwa mhanga wake alikuwa akiuza mihadarati na kwamba alikuwa na silaha. Hata hivyo watu walioshuhudia na wanaharakati wa masuala ya jamii wamepinga ripoti hiyo ya idara ya polisi na kusema kuwa polisi mzungu alitumia nguvu kupita kiasi.
Mauaji hayo ya Rumain Brisbon ni ya hivi karibu zaidi baada ya yale yaliyofanywa dhidi ya Michael Brown huko Missouri, Eric Garner wa New York na Tamir Rice wa Ohio ambayo yote yalifanywa na polisi wazungu dhidi ya Wamarekani weusi.
Uchunguzi uliofanywa na taasisi ya Malcolm X Grassroots Movement, umebaini kuwa Wamarekani weusi 313 waliuawa mwaka 2012 kwa kupigwa risasi na polisi, walinzi binafsi wa usalama na wanachama wa mashirika ya umma na kwamba wahalifu wa kesi nyingi kati ya hizo hawakuchukuliwa hatua yoyote.

No comments: