Saturday, 24 January 2015

BANZA STONE YU MAHUTUTI MJINI TUNDUMA,WASAMARIA WEMA KUJITOLEA KUMRUDISHA DAR

 
Walikwenda mkoani Mbeya na bendi yao Rungwe Music Band (zamani Wana Extra), bendi ikasambaratikia huko kila mtu akarejea Dar na hamsini zake, Banza akaamua kwenda Tunduma na huko ndiko balaa lilipomkumba.
Pengine bado uko kizani. Ni kwamba mwanamuziki nyota wa dansi Ramadhani Masanja “Banza Stone” yuko mahututi mjini Tunduma na hana huduma yoyote ya kimatibabu. 

Kwanini Tunduma? Bendi yao ya Rungwe ilikuwa na ziara katika miji kadhaa ya mkoa wa Mbeya, ziara ambayo haikuwa na mafanikio, jambo lililowalazimisha wanamuziki wa bendi hiyo kurejea jijini Dar es Salaam bila utaratibu maalum.
Wakati baadhi ya wanamuziki wengine wakirejea Dar es Salaam kwa msaada wa mdau wa muziki wa Mbeya mjini Yussuf Fitina, Banza Stone yeye pamoja na wanamuziki wengine wawili akaamua kwenda Tunduma kwa mdau mwingine wa mjini humo anayefahamika kama Brother K, kwa bahati mbaya Banza hakumkuta mwenyeji wake.
Kwa hali hiyo Banza akaanza kuishi maisha ya kubahatisha hapo Tunduma huku ikidaiwa pia kuwa alikuwa akitumia kilevi kwa sana tu, wanamuziki aliokwenda nao huko wakaondoka na kumwacha peke yake ugenini.
Katika siku mbili zilizopita, hali ya Banza ikabadilika, akaanza kuugua, nyumba ya wageni aliyofikia nayo ikamkataa, lakini msamaria mmoja mwanadada anayejitaja kwa jina moja la Nana akabeba jukumu la kumhudumia Banza (japo si kwa kumpeleka hospitali).
Nana amemchukulia Banza chumba katika nyumba ya wageni yenye jina la Palace Lodge.
Katika mazungumzo ya njia ya simu kati ya Nana na mdau wa muziki wa dansi Deo Mutta Mwanatanga wa Dar es Salaam ambayo Saluti5 imefanikiwa kapata ‘clip’ ya maongezi hayo, ni kwamba hali ya Banza inazidi kuzorota badala kuimarika.
“Hali ya Banza si nzuri, leo jioni (jana) alitapika sana na kudondoka,” ilisema sehemu ya mazungumzo hayo ya Nana.
Aidha, katika mjadala mwingine wa wadau wa muziki kupitia makundi ya Whatsapp, Saluti5 ilifanikiwa kupata sehemu ya maelezo ya mtu anayeitwa Rahim ambaye ni kama mtoto wa nyumbani kwa kina Banza – ni ndugu wa hiyari.
Rahim alieleza kama ifuatavyo: “Naitwa Rahim ni mdogo wa Banza kifamilia. Sie ndiye tulikuja nae na band ya Rungwe huku Mbeya, akaniaga kuwa anakwenda Tunduma kuonana na Brother K. “Hali ya Banza ilianza kubadilika tangu yupo Kyela baada ya kuibiwa begi lake lililokuwa na vidonge vyake vya dozi lakini akagoma kuduri Dar,” ndivyo ilivyosema taarifa hiyo ya Rahim. “Kwa sasa mimi niko Mbozi, lakini kesho (leo) mapema nitakuwa Tunduma, najua jinsi ya kuwaelewesha madaktari ili Banza apate matibabu,” iliendelea taarifa ya Rahim.
Kwa mujibu wa Rahim ni kwamba Banza haruhusiwa kupata dawa (za kifua kikuu) hadi kwenye kituo aliachoandikiwa dozi hiyo – Dar es Salaam.
Akiongea na Saluti5, Deo Mutta akasema Nana ameombwa ahakikishe anamsafirisha Banza hadi Mbeya mjini na hapo mipango ya kumrejesha Dar es Salaam itafanyika chini ya mdau Yussuf Fitina.
Hii si mara ya kwanza, wala ya pili, wala ya tatu kwa Banza Stone kuugua hadi kuwa mahututi, lakini bado tatizo sugu la mwanamuziki huyo mwenye washabiki wengi ni kutozingatia masharti ya madktari.
Banza anatakiwa kupumzika, kupata lishe ya maana, kuepuka pombe na vileo vingine lakini vyote hivyo kwake ni vitu visivyowezekana. 
HISANI: SALUTI5


No comments: