Wednesday, 19 November 2014

WACHAFUA MAZINGIRA KUADHIBIWA PAPO HAPO




 Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto imeagizwa kuanza utekelezaji wa utozaji wa faini ya papo kwa papo ya Sh50,000 kwa watakaobainika kuchafua mazingira kwa makusudi.

Agizo hilo lilitolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Magid Mwanga wakati wa kongamano la kuhamasisha usafi na utunzaji wa mazingira lililoandaliwa na Shirika la Wanawake la Utunzaji wa Mazingira Tanzania (YWCA), kupitia Mradi wa Wajibika.

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Ofisa Tarafa ya Lushoto, Asha Hazali, mkuu huyo wa wilaya alisema pamoja na jitihada zinazochukuliwa, ikiwamo kampeni ya kila mwisho wa mwezi ili kuhakikisha mazingira yanakuwa safi wakati wote, bado kuna baadhi ya watu wanakwamisha jitihada hizo makusudi.

“Umefika wakati sasa sheria lazima zianze kutumika, kwani kama ni suala la elimu ya usafi wa mazingira limeshatolewa na viongozi wa Serikali na wanaharakati mbalimbali,” alisema Mwanga.

“Hatuwezi kuendesha maisha kama vile hakuna sheria. Watu wanachafua mazingira na hakuna hatua wanazochukuliwa. Nadhani sasa ni wakati wake,” alisema Mwanga.

Akizungumzia mpango huo, Ofisa wa Wajibika, Carloline Biseko alisema mradi unahusisha zaidi vijana na lengo ni kuwaweka kwenye mstari wa kujitambua.

“Tunahitaji kuona vijana wakiwa na mapenzi na mazingira wanayoishi na kwa kufanya hivyo, watakuwa tayari kuyasafisha,” alisema Biseko.

Biseko alisema mbali na masuala ya mazingira, vijana pia wanaelimishwa juu ya masuala ya ujasiriamali ili watumie fursa zilizopo kujiendeleza kiuchumi. Kongamano hilo lilishirikisha wasanii na wanafunzi wa shule za sekondari.          CHANZO: MWANANCHI

No comments: