Saturday, 22 November 2014
CHANONGO AGOMA KUICHEZEA SIMBA,KISIGA AULILIA UONGOZI
Kiungo wa Simba, Shaban Kisiga ameupigia magoti uongozi wa timu hiyo akiomba umrudishe kwenye timu huku kiungo mshambuliaji, Haruna Chanongo akigoma kuichezea timu hiyo.
Hivi karibuni uongozi wa Simba uliwasimamisha wachezaji watatu, Amri Kiemba, Kisiga na Chanongo kufuatia madai ya utovu wa nidhamu na kucheza chini ya kiwango kwenye mechi dhidi ya Tanzania Prisons katika matokeo ya bao 1-1.
Aidha, kwa upande wa Kiemba, uongozi wa Simba upo katika mazungumzo ya kumuuza mchezaji huyo kwa Azam FC ambapo wanataka walipwe kiasi cha shilingi milioni 15 badala ya milioni 10 wanayoitaka wao.
Kikizungumza na Championi Jumamosi, chanzo cha kuaminika kutoka Simba kimefunguka kuwa, Kisiga ameamua kuuomba msamaha uongozi wa klabu hiyo kufuatia kosa la utovu wa nidhamu alioufanya ambapo tayari amesharudishwa kundini kujiunga na wenzake.
Kilieleza kuwa, kwa upande wa Chanongo, amegoma na hataki kuisikia Simba wala kuichezea tena na badala yake anahitaji aachwe, hivyo kuwapa wakati mgumu viongozi wa timu hiyo.
“Kuhusu Kisiga ishu yake iliisha zamani, aliomba msamaha kwa utovu wa nidhamu alioufanya kwa hiyo ataungana na wenzake mara baada ya kikosi kuanza mazoezi.
“Kwa upande wa Chanongo suala lake linaonekana kuwa gumu, mwenyewe hataki kuichezea Simba, haijajulikana nini hatma yake kwani kuna baadhi ya viongozi wanapendekeza arudishwe Simba B lakini bado hatujaafiki suala lake,” kilisema chanzo hicho.
SOURCE: GPL
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment