Friday, 21 November 2014
MLINZI AGEUKA KUWA NESI KIGOMA
KITUO cha Afya Nguruka wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma kinakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi hali iliyofanya mlinzi wa usiku katika kituo hicho, Boaz Selelo Kiganamo kutumika kama mtoa huduma katika kliniki ya baba, mama na mtoto.
Hali hiyo inatokana na ongezeko kubwa la akinamama wajawazito wanaohudhuria kliniki sambamba na kuwahi kituo cha afya wakati wa kujifungua ikiwa ni matokeo ya kampeni inayojulikana kama Thamini uhai okoa maisha ya mama na mtoto inayoendeshwa na Shirika la World Lung Foundation.
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Nguruka, Staford Chamgeni amekiri kuwepo ongezeko kubwa la akinamama wajawazito na watoto wanaohudhuria kwenye kituo na kubainisha kwamba ongezeko halilingani na ikama ya watumishi waliopo.
“Kwa kweli kwa sasa idadi ya kina mama wajawazito ni kubwa na hiyo imefanya tukabiliwe na mzigo mzito wa kuwahudumia na ndiyo maana hata watumishi wa idara nyingine wanalazimika kufanya kazi ya kusaidia katika Idara ya Kliniki,” alisema Mganga huyo Mfawidhi.
Akizungumzia hali hiyo mlinzi huyo alisema kuwa baada ya kumaliza zamu yake ya ulinzi usiku analazimika kusaidia kufanya kazi kwenye kliniki ya baba, mama na mtoto kutokana na upungufu mkubwa wa watumishi uliopo kwani wahudumu waliopo wame kuwa wakikabiliwa na mzigo mkubwa wa watu wanaofika kupata huduma kituoni hapo.
Kwa upande wake Maria Josephat, Muuguzi katika Kituo cha Afya Nguruka alisema kuwa ongezeko kubwa la akinamama wajawazito wanaofika kituoni hapo kupata huduma limewalazimu kufanya kazi masaa mengi ili kuendana na hali hiyo.
Hata hivyo alisema kuwa licha ya hali hiyo wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la kutopata malipo yao ya kufanya kazi saa za ziada kwa wakati na pengine kutopata kabisa na kwamba pamoja na hilo hawajakata tamaa katika kuwahudumia akinamama hao.
Kwa sasa kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa kituoni hapo zinaonesha kuwa zaidi ya akinamama wajawazito 200 hufika kujifungua kituoni hapo kwa mwezi kuanzia Septemba mwaka huu kutoka akinamama kati ya 80 na 130 waliokuwa wakijifungua kwa mwezi kabla ya zoezi hilo la uhamasishaji.
Akieleza mafanikio yaliyopatikana kutokana na kampeni hiyo, Anna Zakaria, Muuguzi Mkunga katika chumba cha upasuaji kituoni hapo alisema kuwa kufuatia kampeni hiyo kumekuwa na mafanikio katika kupunguza idadi ya akinamama wanaojifungua kwa njia ya upasuaji kutoka akinamama saba hadi 10 na kufikia akinamama 3 hadi 5.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Albert Mumwi amekiri kuwepo kwa upungufu mkubwa wa watumishi kwenye vituo vya utoaji huduma na kwamba kwa sasa kliniki za baba, mama na mtoto zimekuwa na ongezeko kubwa ambalo haliendani na idadi ya watumishi waliopo.
Mumwi alisema kuwa kutokana na hali hiyo Halmashauri imekuwa ikitoa posho ya kufanya kazi saa za ziada ingawa bado hata kiasi
kinachotengwa hakitoshelezi idadi ya watoa huduma wanaopaswa kulipwa.
CHANZO: HABARI LEO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment