Friday, 21 November 2014
WAASI WA KUSINI MWA SUDAN WATAKA KUJITAWALA
Waasi wa Sudan wanataka majimbo mawili yaliyogubikwa na machafuko huko kusini mwa nchi hiyo ya Kordofan Kusini na Blue Nile yapewe mamlaka ya ndani ya kujitawala. Hayo yameelezwa na Yasir Arman mkuu wa jopo la waasi kwenye mazungumzo ya amani na serikali ya Sudan. Arman ameelezea sababu kuu ya kutaka kupewa mamlaka ya ndani kwa kusema kuwa, majimbo hayo yanakaliwa na idadi kubwa ya Wakristo, hivyo mila na utamaduni wa wakazi wa majimbo hayo inatofautiana mno na wakazi wa majimbo mengine ya Sudan. Yasir Arman ameongeza kuwa, wakazi wa maeneo ya Darfur, eneo la mashariki mwa Sudan na jimbo la al Jazira wana haki pia ya kuwa na mamlaka ya ndani ya kujitawala, ili waweze kuendesha mambo yao kwa uhuru zaidi. Inafaa kuashiria hapa kuwa, Sudan Kusini ambayo kabla ya kujipatia uhuru ilikuwa ikijulikana kama kusini mwa Sudan, mwaka 2011 ilitangaza kujipatia uhuru wake baada ya kufanyika kura ya maoni ya kuainisha mustakbali wa eneo hilo lenye majimbo kumi. Licha ya Sudan Kusini kujipatia uhuru lakini nchi hiyo bado inashuhudia machafuko na mapigano ya ndani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment