Friday, 21 November 2014
UN YATAKA MFÀNYAKAZI WAKE KUACHIWA HURU
Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kuachiwa huru mfanyakazi wake aliyetekwa nyara na kupelekwa kusikojulikana nchini Sudan Kusini.
Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) linalowasaidia maelfu ya raia walioathiriwa na vita kwa kipindi cha karibu mwaka mmoja sasa huko Sudan Kusini limetangaza kuwa, lina wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya Mark Diang ambaye alitekwa nyara na genge la watu waliokuwa na silaha Oktoba 16 katika uwanja wa ndege wa mji wa Malakal. Mkuu wa WFP nchini Sudan Kusini, Joyce Luma amesema, kutekwa nyara na kutoweka kwa Mark Diang kumekuwa na taathira mbaya kwa wafanyakazi wenzake ambao sasa baadhi yao wanashindwa kufanya kazi kwa kuhofia maisha yao.
Wafanyakazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa wamekuwa wakitekwa nyara au kuuawa mara kwa mara katika nchi iliyokumbwa na vita vya ndani ya Sudan Kusini. Mwezi Agosti mwaka huu pekee watu waliokuwa na silaha walishambulia na kuwaua wafanyakazi wasiopungua 6 wa Umoja wa Mataifa nchini humo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment