Tuesday, 9 December 2014
POLISI AMTETEA MTUHUMIWA MAHAKAMANI KISUTU
KESI ya kughushi inayomkabili mfanyabiashara, Hans Aingaya Macha imechukua sura mpya, baada ya askari Johanes Mgendi mwenye namba E 2982 kutoa ushahidi katika upande wa mtuhumiwa kwenye kesi hiyo.
Mgendi ambaye ni mtaalamu wa maandishi Makao Makuu ya Polisi mjini Dar es Salaam, alitoa ushahidi huo mwishoni mwa wiki katika kesi hiyo iliyopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu chini ya Hakimu, Devotha Kisoka.
Askari huyo, alidai nyaraka alizochunguza amebaini miandiko inafanana na kuomba mahakama ipokee ushahidi wake, katika kesi hiyo inayomkabili mfanyabiashara huyo mahakamani hapo.
“Haya ni maoni yangu, nililetewa jalada la uchunguzi na askari wa Kituo Kikuu cha Polisi kuchunguza suala hilo na kutoa maoni hayo,’’alidai askari huyo na kumfanya wakili wa serikali, Nassoro Katuga kutikisa kichwa.
Hata hivyo, Katuga alimuuliza swali askari linalohusu taarifa ya uchunguzi wa suala hilo ya mwanzo iliyofanywa na Mkuu wa Idara ya Uchunguzi, Amaan Renatus Saad na kuonesha saini zimeghushiwa.
Saad alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Uchunguzi wa Maandishi Makao Makuu ya Polisi nchini.
Swali hilo, lilimfanya askari huyo aliyekuja mahakamani kumtetea Macha kudai kuwa katika Polisi hakuna ukubwa huku akisisitiza kuwa yale ni maoni yake yeye na hayahusiani na Amaan, ambaye tayari alishatoa ushahidi kwa upande wa serikali.
Hakimu wa mahakama hiyo, aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 22, mwakani kwa ajili ya kutoa hukumu. Macha anashitakiwa kwa kosa la kughushi hati, mkataba wa mauziano na kuwasilisha hati ya umilikishaji miliki kwa Msajili wa Hati.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment