Tuesday, 9 December 2014

HOUSEGIRL ANUSURIKA KIFO


Msaidizi wa kazi za ndani (hausigeli), Rehema Ally (17), mkazi wa Yombo, Machimbo Mwisho, Ilala jijini Dar, amechanwachanwa kwa wembe na kisu sehemu mbalimbali za mwili wake, hali iliyosababisha alazwe katika Hospitali ya Amana kwa matibabu.


Akizungumza na Uwazi nyumbani kwa mwajiri wake aliyejulikana kwa jina moja la Ghati, Yombo jijini Dar, Rehema aliyefika jijini hapa Januari, 2013 akitokea nyumbani kwao, Masasi mkoani Mtwara, alikuwa na haya ya kusema: 
“Nakumbuka siku hiyo ilikuwa ni Jumapili ya Novemba 30, saa moja usiku nikiwa nje ya nyumba ya bosi wangu. Akatokea msichana mmoja aitwaye Fatuma na mwenzake aitwaye Ashura huku wakiwa wamebeba kisu na wembe. Wakanikamata kwa nguvu na kunikaba, wakaniangusha chini na kuanza kunichanachana mwili mzima.
“Wakati huo nilikuwa naelekea nyumbani kwa akina Fatuma kuchukua sanduku langu ambalo alilichukua kwa bosi wangu akidai kwamba nimempotezea ‘memori kadi’ ya simu yake hivyo alisema kwamba mpaka nitakapomrudishia ndipo nitakapochukua sanduku langu.

“Walinijeruhi sana na kukimbia, nikarudi ndani lakini bosi wangu hakuwepo nyumbani na aliporudi alinichukua na kunipeleka polisi, tukapewa kibali cha matibabu (PF3) na kwenda Hospitali ya Amana kutibiwa. Tulirudi nyumbani na baadaye tukafuatilia kesi yetu polisi, wakasema turudi nyumbani tukaelewane mbele ya mjumbe ili kesi imalizike.
“Tulienda kwa mjumbe pamoja na Fatuma na wazazi wake na mimi nilikuwa na bosi wangu, wakataka kesi imalizike yaani tusameheane lakini kwa upande wa wazazi wangu waliopo Masasi, nilipowapa taarifa walikataa kumaliza kesi kienyeji na kutaka ifike mahakamani kwa vile watuhumiwa walikuja na silaha na walidhamiria kuniua,” alisema Rehema.
Kwa upande wa mtuhumiwa, Fatuma Zuberi (17), alipoulizwa na waandishi wetu, alidai kwamba wakiwa njiani na mdogo wake wakienda dukani kununua vocha, walivamiwa na Rehema na kushambuliwa akitaka wamrudishie sanduku lake.

Naye mama mzazi wa Fatuma aliyejitambulisha kwa jina la Sharifa Mwinyi Kondo, alidai kwamba mwanaye pia amejeruhiwa hivyo waliamua mambo yote yaishe kwa kusameheana mbele ya mjumbe wao. Mjumbe wa shina namba 22, Rose Kiravu alipoulizwa kuhusu ishu hiyo alikiri kupokea taarifa hizo na kudai kwamba suala hilo lilifika polisi lakini lilirudishwa kwake kwa upatanishi ambapo alikaa na pande zote mbili pia wajumbe wa nyumba kumi wawili na wote waliamua kusameheana.

No comments: