Watu 6 wamefariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa wilayani Songea mkoani Ruvuma baada ya kupigwa na radi kufuati mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia Jumamosi..
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma ACP Mihayo Msikhela amesema kuwa maafa hayo yalitokea majira ya saa mbili usiku wakati watu hao wakila chakula cha usiku kwenye mgahawa wa chuo cha kilimo na mifugo cha Liti Madaba Songea
Kamanda huyo ameongeza kuwa mvua kubwa ilinyesha majira ya saa moja na nusu hadi saa mbili na baadaye ikapiga radi na kuua watu sita na kujeruhi watu wawili.
Amewataja waliopoteza maisha kwa kupigwa na radi kuwa ni Chesco Luoga mwanafunzi wa chuo cha Liti Madaba na mkazi wa Ludewa, Lucas Mabula mwanafunzi wa chuo hicho na mkazi wa Magu mkoani Mwanza, Eva Chapile muhudumu wa mgahawa wa chuo hicho, Osiana Antoni mhudumu wa Mgahawa wa chuo hicho, Justine Ngonyani mkulima na mkazi wa madaba Songea na Edwini Fungo mkulima na mkazi wa Madaba Songea.
Amewataja majeruhi kuwa ni Beatrice Mhagama mwanafunzi wa chuo cha Kilimo na mifugo Liti Madaba na mkazi wa Peramiho Songea na Leokadia Fusi muhudumu wa mgahawa wa chuo hicho na kwamba miili ya marehemu na majeruhi wako katika kituo cha afya Madaba.
Kutokana na tukio hilo mkuu wa mkoa wa Ruvuma Bw. Said Mwambungu na Mkuu wa wilaya ya Songea Bw.Joseph Mkirikiti wameenda eneo la tukio Madaba Songea na kueleza kusikitishwa na tukio hilo na kusema huo ni msiba mzito kwa mkoa wa Ruvuma.
No comments:
Post a Comment