Tuesday, 25 November 2014

MOROCCO YAWAKAMATA WAPIGANAJI WA DAESH


Washukiwa sita wametiwa mbaroni nchini Morocco baada ya mkanda wa video kuwaonyesha wanaume sita waliovalia maski wakitangaza utiifu wao kwa kundi la kigaidi la Daesh, linalozusha hofu na wasiwasi huko Iraq na Syria. Watu watatu walitiwa mbaroni jana na wengine watatu hapo jana. Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Morocco imeeleza kuwa, mkuu wa kundi hilo na washirika wenzake wawili walifungwa jela mwaka 2008 nchini humo kwa kuhusika katika njama za ugaidi na kuwa na uhusiano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida.

Vikosi vya usalama na polisi wa Morocco wamenasa pia simu ya mkononi iliyokuwa ikitumiwa na magaidi hao kurekodia picha za video na visu alivyokuwa navyo mmoja wa washukiwa hao. Watu hao sita waliotangaza utiifu wao kwa kundi la kitakfiri la Daesh wametiwa mbaroni baada ya ripoti za vyombo vya habari kueleza kuwa, mkanda ulioonyeshwa wiki iliyopita, ulirekodiwa huko Morocco. Mkanda huo wa video uliwaonyesha wanaume watatu wakiwa na bendera ya Daesh huku wakijiarifisha kuwa wanachama wa kundi hilo la kigaidi.

No comments: