Tuesday, 25 November 2014

MAKINDA AWA MBOGO SAKATA LA ESCROW


SPIKA wa Bunge, Anne Makinda amerejea bungeni kwa kishindo, baada ya jana kukataa pendekezo la kusitisha kazi nyingine za Bunge kujadili taarifa ya kukamatwa kwa baadhi ya watu wanaodaiwa kusambaza ripoti kuhusu akaunti ya Tegeta Escrow ya IPTL.

Aidha, amesema wabunge watamuonesha ni kwa jinsi gani amehongwa Sh bilioni 1.6 (Dola za Marekani milioni moja) katika sakata hilo.

Akiongoza Bunge kwa mara ya kwanza katika Mkutano wa 16 na 17 baada ya kuwa safarini kwa muda mrefu, Makinda pia ameahidi kuwa wabunge watapewa ripoti hiyo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuhusu sakata la fedha za IPTL.

Alitoa maelekezo hayo baada ya Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), kuomba kupitia Kanuni za Bunge, shughuli za Bunge zilizopangwa zisiendelee badala yake wabunge wajadili kusambazwa kwa nyaraka za CAG zinazodaiwa kuibwa ofisini kwa Spika.

Mbatia alisema kumekuwapo na taarifa za mtu kudurufu ripoti hiyo na kuisambaza kwa wabunge na watu mbalimbali, jambo ambalo ni kinyume cha Kanuni.

Hivyo, kwa kutumia Kanuni za Bunge, alitaka Spika asitishe shughuli nyingine na jambo hilo lijadiliwe.

“Kazi ya Bunge ni kuisimamia Serikali, sasa hili linashusha hadhi ya Bunge isifanye kazi yake vizuri, kwa hiyo napendekeza tulijadili hapa. Naomba mambo mengine yasitishwe, tulijadili,” alisema Mbatia.

Lakini Makinda licha ya kumpongeza Mbatia kwa kulieleza hilo, alithibitisha kuwa Polisi wanamshikilia mtu mmoja kuhusu suala hilo, lakini akawahoji wabunge kwamba sasa wanataka kujadili nini.

“Sasa mnataka tujadili nini? Hatuendeshi Bunge bila taratibu. Mmeandika ninyi hizo nyaraka? Ofisi yangu imedhalilishwa. Lakini hili tayari liko Polisi, linashughulikiwa na wenzetu hawa. “Watamhoji huyo mtu alipata wapi nyaraka hizo na kuna mahali walipochapia Dar es Salaam wataenda ku-confiscated (kutaifisha). Kwa hiyo, hapa hakuna la kujadili, labda wangekuwa wamemaliza kazi yao ya uchunguzi,” alisema Makinda huku baadhi ya wabunge wakiendelea kumbana.

Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mohamed Mnyaa (CUF), alipopewa fursa ya kuzungumza , alidai kuwa suala hilo ni vyema likajadiliwa kwani kuna nyaraka zaidi zinawekwa katika makazi ya wabunge na usalama wao uko hatarini.

Mnyaa alikwenda mbali zaidi na kumweleza Spika kuwa “ipo minong’ono pia inakuhusisha nawe Spika kwamba umehongwa Dola za Marekani milioni moja. Sasa ni bora tukajadili suala hilo,” alisema Mnyaa.

Ni kama alikuwa amemtonesha zaidi Spika Makinda, kwani alikuja juu na kusema: “Mtanionesha, mtanionesha, mtanionesha hizo hela. Hatuwezi kufanya mambo ya kitoto.”

Akimjibu Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, Makinda alisema ni vyema wote wenye nyaraka hizo wakazirudishe Polisi.

Akijibu ombi la Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM) la kutaka ripoti hiyo ya CAG na vielelezo vyake kupewa wabunge mapema ili kujiandaa na mjadala, Spika alisema utaratibu unaandaliwa.

Akichangia mjadala wa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2014, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), alisema mtu aliyekamatwa akisambaza nyaraka hizo ana uhusiano wa karibu na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.

Alisema kuwa polisi wanataka kumpeleka mtuhumiwa huyo mahakamani ili baadaye Bunge lizuiwe kujadili suala lake kwa kuwa litakuwa limefikishwa katika mhimili huo mwingine wa Dola, hivyo kikanuni watazuiwa kulizungumzia bungeni.

Ripoti ya CAG ilikabidhiwa bungeni na Serikali, Novemba 14, mwaka huu na kisha Bunge iliikabidhi kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) siku tatu baadaye, kwa ajili ya uchambuzi na maoni kabla ya kuwasilishwa ndani ya Bunge.

Kamati hiyo ya PAC inaendelea na vikao vyake na kwa mujibu wa ratiba ya Bunge, mjadala wa ripoti hiyo utaanza kesho na unatarajiwa kuendelea kabla ya Bunge kuahirishwa Ijumaa wiki hii.

Akaunti hiyo ilifunguliwa katika Benki Kuu yaTanzania (BoT) baada ya kuwapo kwa mgogoro wa kibiashara wa Tanesco na IPTL, kampuni inayofua umeme yenye mitambo yake Tegeta, Dar

No comments: