Wednesday 26 November 2014

SASA NI ZAMU YA WAKAZI WA BAGAMOYO KUPONDA MARAHA BAHARINI


“Kivuko hiki ndicho bora kuliko vyote kati ya 27 tulivyonavyo nchi nzima. Kitabeba watu zaidi ya 500 ukijumlisha na wengine watakaokuwa wamesimama”

Usafiri wa majini una raha yake, hasa ikiwa chombo unachotumia ni imara na chenye usalama usiotiliwa shaka.

Wasafiri kati ya Dar es Salaam na Zanzibar ni mashuhuda wa baadhi ya vyombo vya majini vyenye mvuto wa aina yake. Ukiwa katika vyombo hivi utafurahia mwonekano wake, mwendo na sifa nyinginezo.

Kwa watu wengi hasa wanaotumia vyombo hivi, usafiri katika maeneo hayo ni zaidi ya safari. Ni utalii wa aina yake.

Ukiondoa raha ya wasafiri wa Dar es Salaam na Zanzibar, sasa ni zamu ya wakazi wa Dar es Salaam na Bagamoyo. Kwa wasiotaka usafiri wa barabara, Serikali imewaletea usafiri wa majini. Kivuko cha Mv Dar es Salaam, kimewasili nchini tayari kutoa huduma ya usafiri kati ya maeneo hayo.

Pamoja na kivuko hicho kuelezwa kuwa kitasaidia kupunguza msongamano wa magari, matumizi yake yanaweza pia kuchukua sura ya utalii

“Hiki kivuko kitakuwa na matumizi mengi, wengine watapenda kufungia ndoa humo, wengine watakuwa wakitalii. Naomba Watanzania wakitunze ili kidumu,” anasema Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.

Mv Dar es Salaam

Katika hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2013/14, Dk Magufuli alitaja miradi mbalimbali itakayosaidia kupunguza foleni katika jiji hili. Miongoni mwa miradi hiyo ilikuwa ni ujenzi wa kivuko kitakachofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo.

Novemba 17, mwaka huu kivuko hicho kiliwasili nchini kutoka Bangladesh baada ya safari ya siku 14 kikiwa chini ya usimamizi wa mkandarasi, Kampuni ya Johs Graham-Hanssen M/S ya Denmark.

Dk Magufuli anasema kivuko hicho chenye thamani ya Sh7.9 bilioni, kina mwendo wa kasi zaidi kuliko kivuko chochote nchini na kina uwezo wa kubeba watu 300 waliokaa, huku wengine wakisimama.

Anasema kivuko hicho pamoja na miradi mingine kama vile ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka (BRT), barabara za pembeni na barabara za juu, kitasaidia kupunguza msongamano wa magari ambao umekuwa sugu kwa sasa.
Chanzo: Mwananchi

No comments: