Saturday, 29 November 2014
HATIMAYE RAIS KIKWETE ATAJWA KUHUSIKA SAKATA LA ESCROW...SOMA UHUSIKA WAKE HAPA CHINI
Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu amemtaja Rais Jakaya Kikwete kuwa sehemu ya mgogoro mzima wa Kampuni ya kufua umeme ya IPTL tangu ilipoingia nchini mwaka 1994.
Akichangia Ripoti ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) alisema ilijulikana miaka 20 iliyopita kwamba IPTL itakuja kuwaumiza Watanzania.
“Mwaka 1994 wakati IPTL wanaandika MoU (makubaliano ya awali) na Serikali, Waziri wa Nishati na Madini alikuwa Kanali Jakaya Kikwete, mwaka 1995 wakati mkataba wa kununua umeme unasainiwa kati ya Serikali na wawekezaji hawa, Waziri wa Fedha alikuwa mtu aitwaye, Kanali Jakaya Mrisho Kikwete.
“Miaka 20 baadaye Sh321 bilioni za Watanzania zimeibiwa, Rais wa Tanzania ni Jakaya Mrisho Kikwete, tunataka fedha zetu zirudi,” alisema Lissu.
Mara baada ya kauli hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk Mary Nagu alisimama na kuomba mwongozo kuhusu matumizi ya jina la rais bungeni.
Akisoma vifungu vya mwongozo wake, Nagu alisema mbunge hatatumia jina la Rais kwa dhihaka katika mjadala au kwa madhumuni ya kutaka kulishawishi Bunge kwa madhumuni fulani na mbunge hataweza kuzungumzia mwenendo wa Rais, jaji, spika au mtu yeyote hadi pale kukiwa na hoja husika.
“Hivi kweli humu ndani lazima tuitane wezi au kutumia lugha za maudhi? Lazima humu ndani tutumie lugha za staha na tukafikia uamuzi utakaoheshimika na watu wote,” alisema Nagu.
Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu aliyekuwa akiendesha kikao cha jioni alisema: “Nakubaliana na hoja ya waziri ni kweli kanuni zinatuzuia kutumia maneno ya watu vibaya, tusitumie majina ya Rais, mahakimu, majaji au majina yoyote.
Akihitimisha mchango wake, Lissu alisema: “Sijatumia jina la Rais vibaya, ila nilichosema ni ukweli mtupu kuwa kipindi wanakuja (IPTL) Rais wetu alikuwa waziri wa nishati, wakati wanasaini makubaliano alikuwa waziri wa fedha na wakati fedha zinachotwa Rais wetu ni Kikwete.”
Akizungumzia sakata hilo Lissu alisema: “Ni aibu waziri kupewa Sh1.6 bilioni... hakuna jambo baya kama mwanasheria mkuu wa zamani kupewa hongo ya Sh1.6 bilioni, hakuna jambo baya viongozi wetu wa dini kupewa hongo, sasa sisi tunazungumza mambo mabaya yanayotokea, hakuna mambo mabaya kama hakimu, jaji kupewa Sh400 milioni sehemu ambako kesi ilikaa kwa muda mrefu na hakuna jambo baya kama fedha kuibiwa,” alisema Lissu.
Kuhusu fedha hizo ni mali ya nani, Lissu alisema: “Fedha hizi ni za wananchi na nchi hii, TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania), CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) wote wamesema ni fedha za umma, Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) wamesema ni fedha za umma lakini watu pekee wanaosema siyo fedha za umma ni wale waliokula.
“Mpaka majaji, viongozi wa umma, viongozi wa dini, wanasiasa wamegawana, tunaambiwa katika mifuko... lazima watu wawajibike kwa hili. Tuanze na hawa tunaowaweza ambao ni Waziri Mkuu (Mizengo Pinda), Mwanasheria Mkuu (Frederick Werema), Tibaijuka (Profesa Anna, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), Chenge (Mbunge wa Bariadi, Andrew), Ngeleja (Mbunge wa Sengerema, William) yaani majizi yote yaliyomo humu tuyawajibishe,” alisema Lissu.
Aliongeza: “Waziri Mkuu lazima awajibike kwa kuwa alikuwa anajua kinachoendelea na alinukuliwa na karibu barua zote, sasa kamati imesema Waziri Mkuu awajibike kwa sababu ndiye anayesimamia shughuli za Serikali za kila siku.”
Lissu aliyetumia dakika 30 kuchangia ripoti hiyo baada ya mbunge mwingine kumwachia muda wake, alisema kuna Usalama wa Taifa chini ya Rais, kitengo cha upelelezi cha Wizara ya Fedha, vyombo ambavyo vilitakiwa kuzuia lakini havikutimiza wajibu wake.
“Tunamwacha mkuu wa usalama wa taifa, tunamwacha waziri wa fedha, tunamwacha katibu mkuu wa wizara ya fedha, tunamwacha gavana wa Benki Kuu ambao wote kwa pamoja walishindwa kutekeleza wajibu wao hadi fedha hizi zilipotolewa,” alisema Lissu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment