Wednesday, 26 November 2014

OBAMA AMPA POLE JK


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete mchana wa Jumatatu, Novemba 24, 2014 amepokea salamu za pole kutoka kwa Rais wa Marekani Mheshimiwa Barak Obama.

Katika salamu zake Rais Obama ameelezea kufurahishwa na taarifa kwamba Rais Kikwete anaendelea vyema kiafya baada ya kufanyiwa upasuaji kwa mafanikio na kuondoa tatizo la tezi dume alilokuwa nalo.

Rais Obama amesema katika salamu hizo kuwa alipata heshima kufanya ziara rasmi nchini Tanzania mwaka 2013, na pia kumualika Rais Kikwete kwenye mkutano wa  Marekani na viongozi wa Afrika mwaka huu.

“Nakutakia kasi ya kupona kabisa na nataraji kuendelea kufanya kazi nawe katika masuala tuliyokubaliana ya kipaumbele”, amesema Rais Obama kwenye salamu zake hizo.

Rais Kikwete amekabidhiwa salamu hizo na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Mhe. Liberata Mulamula, aliyekuwa ameongozana na maafisa waandamizi wa ubalozi waliofika Baltimore kumjulia hali.

Mhe. Mulamula amesema salamu kutoka sehemu mbalimbali duniani zimekuwa zikimiminika ubalozini kwa njia mbalimbali.

Taratibu za matibabu za Mheshimiwa Rais Kikwete zilikamilika Jumatatu, Novemba 24, 2014 asubuhi baada ya  madaktari bingwa katika Hospitali ya Johns Hopkins iliyoko mjini Baltimore, Jimbo la Maryland, Marekani, kumfanyia  hatua ya mwisho ya tiba.

Rais Kikwete ameendelea kupumzika na kuangaliwa kwenye Hoteli Maalum inayohusiana na Hospitali ya Johns Hopkins kwa siku tatu kabla ya kuanza safari ya kurejea nyumbani.

Kama kila kitu kitakwenda kama ilivyopangwa na madaktari, Rais Kikwete anatarajiwa kurejea nyumbani Jumamosi, Novemba 29, 2014.

Rais Kikwete aliondoka nchini Alhamisi ya Novemba 6, 2014, kwenda kufanyiwa uchunguzi wa afya yake lakini madaktari katika Hospitali ya Johns Hopkins waliamua kumfanyia upasuaji wa tezi dume Jumamosi ya Novemba 8, 2014.

Rais Kikwete anaendelea kuwashukuru Watanzania kwa sala na maombi yao ya kumtakia heri ya kupona haraka na kurejesha afya njema katika kipindi chote cha ugonjwa wake.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu – Dar es Salaam.

25 Novemba,2014

No comments: