Tuesday, 25 November 2014

NAMBA ZOTE ZA SIMU KUSAJILIWA UPYAAAAAAAAAAAAA


SERIKALI imesema itafanya tena usajili wa namba zote za simu za mkononi nchini ili kuthibitisha zinazotumika.

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba alisema hayo bungeni jana wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge kupitia Baraza la Wawakilishi, Jaku Hashim Ayoub (CCM).

January alikiri ni kweli kuwa wapo watu wanaotumia majina feki katika kusajili namba zao za simu za mkononi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

“Wapo watu wanaotumia majina na vitambulisho feki wanaposajili namba zao. “Tunaomba waheshimiwa wabunge mtuunge mkono tutakapotangaza usajili mpya wa namba za simu,” alisema Naibu Waziri January.

Aidha, alisema Serikali inakusudia mwakani kuwasilisha muswada wa kutunga sheria tatu ili kudhibiti usalama katika mitandao ya mawasiliano.

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), Naibu Waziri alikiri kuwapo kwa utapeli kwa kutumia mitandao ya intaneti, pia akakiri uwezo mdogo wa vyombo vya ulinzi na usalama katika kuchunguza, kubaini na kudhibiti matumizi hayo.

Alisema sheria zinazopendekezwa zitadhibiti hali hiyo. Katika swali lake la nyongeza, Mdee alisema kumekuwapo na uhalifu wa kutumia mitandao ya intaneti na kuwataja waliowahi kuhusishwa katika utapeli huo kuwa ni yeye mwenyewe, wabunge Kabwe Zitto na Edward Lowassa na Kampuni ya IPP.

Akijibu swali la msingi la Ayoub, Naibu Waziri January alisema kwa mujibu wa sheria, ni kosa la jinai kutumia au kuwezesha kutumika Sim Card isiyosajiliwa. Alisema atakayebainika anatumia atapewa adhabu ya faini ya Sh 500,000 au kifungo cha miezi mitatu jela.

Pia muuzaji yeyote atakayebainika kuuza Sim Card ambazo hazijasajiliwa atakuwa ametenda kosa la jinai, na atalipa faini ya Sh milioni tatu au kifungo cha miezi 12 au adhabu zote zinaweza kutekelezwa kwa pamoja.

No comments: