Wednesday, 17 December 2014
UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA: AFUKUZWA BAADA YA KUMSHINDA BABA MWENYE NYUMBA
VITUKO vinazidi kuripotiwa katika chaguzi za serikali za mitaa zinazoendelea nchini na mjini Morogoro, mgombea kutoka muungano wa Ukawa, Sharrif Abdul Mnola (Chadema) ametimuliwa kwenye nyumba aliyokuwa anaishi baada ya kumshinda mpinzani wake, Makalla Salum Hassan (CCM) ambaye ni mmiliki wa mjengo huo uliopo mtaa wa Ngoma ‘A’ kata ya Mji Mpya.
Sharrif ambaye ni dalali wa magari alishinda baada ya kupata kura 79 huku Makalla akipata 72.
Mara baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, kundi la vijana wakiwa na magari na bodaboda, walimbeba juujuu Sharrif na kuanza maandamano hadi nyumbani kwake ambako mwenye nyumba huyo alikuwa amejifungia chumbani kwake kuepuka kelele za watu hao waliokuwa wakiimba kwa kutaja neno Escrow.
Inadaiwa kuwa kitendo cha wafuasi wa Sharrif kumfuata nyumbani kwake na kumzomea Makalla kilimkera sana na kukiona kama cha kupangwa na mshindi, hivyo kwa namna hiyo, hataweza tena kuishi na mpangaji wake huyo kwa amani.
Akizungumzia uchaguzi huo kabla ya taarifa za kufukuzwa kwake ndani ya nyumba hiyo kuripotiwa, Sharrif alisema ulikuwa mgumu na kwamba kilichomfurahisha ni kwa mpinzani wake kukubali matokeo kwa kitendo chake cha kusaini fomu maalum za kukubali kushindwa.
Makalla mwenyewe hakuweza kupatikana kuthibitisha habari hizo licha ya kupigiwa simu mfululizo kwenye simu yake ya mkononi.Katika uchaguzi huo kwenye kata ya Mji Mpya wenye mitaa 12, CCM ilishinda mitaa kumi, Ukawa mmoja na matokeo ya mtaa mmoja hayakutangazwa baada ya mawakala wa Ukawa kukataa kusaini fomu ya matokeo kufuatia ongezeko la kura 14 wakidai kuwepo kwa mchezo mchafu.
Chanzo:Gpl
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment