Saturday 20 December 2014

PLUIJM ASAINI MWAKA MMOJA NA NUSU KUINOA YANGA


       Kocha Mholanzi wa Yanga, Hans van Der Pluijm.
WAKATI kocha Mholanzi wa Yanga, Hans van Der Pluijm akisaini mkataba wa mwaka mmoja na nusu kuinoa Yanga jana, Mbrazili aliyefungashiwa virago, Marcio Maximo juzi usiku alikabidhiwa kitita chake cha dola 12,000 (zaidi ya Sh milioni 20) na kumalizana kabisa na Yanga.
Pluijm aliyetua kuifundisha timu hiyo Jumatatu ya wiki iliyopita, amesaini mkataba huo baada ya Yanga kumalizana na Maximo ambaye wamempa mshahara wake wa mwezi mmoja kama walivyokubaliana kimkataba. 

Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya kamati ya utendaji ya timu hiyo, Pluijm amesaini mkataba huo baada ya kufikia makubaliano na mwenyekiti Yusuf Manji. “Pluijm tumemalizana naye baada ya mazungumzo ya muda mrefu kabla ya kukubali kusaini mkataba wa kuifundisha Yanga.
“Tumeingia naye mkataba wa mwaka mmoja na nusu, baada ya pande zote mbili kukubaliana na kufikia muafaka wa kumpa mkataba huo, lengo kubwa timu yetu ifanye vizuri katika mzunguko wa pili wa ligi kuu.
“Na kesho (leo) asubuhi Pluijm anatarajiwa kuanza kazi rasmi ya kukinoa kikosi chetu akiwa na msaidizi wake Mkwasa (Charles) kwenye Uwanja wa Loyola,” kilisema chanzo hicho.
Katika hatua nyingine, ofisa habari mpya wa timu hiyo, Jerry Muro, alisema wamemshukuru Maximo na msaidizi wake, Leonardo Neiva kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha katika kipindi cha miezi sita walichoifundisha Yanga.
“Ninaomba nichukue fursa hii kumshurukuru Maximo na msaidizi wake Neiva kwa ushirikiano waliouonyesha kuifundisha Yanga kwa kipindi cha miezi sita, hivyo tunawatakia kila la kheri katika safari yao na Mungu akipenda tutaendelea kushirikiana siku za mbele,” alisema Muro.
Maximo anatarajiwa  kuondoka nchini kurudi kwao Brazil kesho Jumapili.
Muro alitangaza sekretarieti yao mpya iliyopendekezwa na kamati ya utendaji ya timu hiyo, ambayo itaongozwa na katibu mkuu, Jonas Tiboroha, Omar Kaya yeye atahusika na masoko, Frank Chacha ataiongoza idara ya sheria na Baraka Deusdedit atakuwa bosi wa fedha.
Katika hatua nyingine, Pluijm ameweka bayana kuwa, straika Emmanuel Okwi hakuwa na mapenzi ya dhati na Yanga, ndiyo maana alikuwa akifanya vimbwanga mara kwa mara.
 “Sijamuona akicheza kwa sasa, lakini naamini kama atapata anachokitaka, hakika ana kiwango kizuri na ataisaidia timu anayoipenda,” alisema Pluijm.
“Sidhani kama Okwi alikuwa na mapenzi ya dhati na Yanga, hakuwa na furaha ndiyo maana aliamua kuondoka mwenyewe, hicho ndicho kitu nilichomfahamu Okwi.”

No comments: