Hatma iwapo mashindano ya Miss Tanzania yataendelea au yatasitishwa kwa muda, itategemea majibu ya tathmini iliyofanyika mwishoni mwa wiki jana yanayotarajiwa kutolewa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) wiki chache zijazo.
Tathmini hiyo iliyowahusisha viongozi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Basata, TGNP, wadau wa sanaa na mashirika mbalimbali, ilibaini ukiukwaji wa kanuni na mwongozo wa mashindano hayo kwa mwaka 2014.
Kaimu Katibu Mkuu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza aliliambia gazeti hili kuwa, iwapo Kamati ya Miss Tanzania ikakutwa na makosa zaidi, huenda wakapewa muda wa kujitathmini na kujipanga upya kama ilivyokuwa kwa Miss Utalii, kwani wamevunja kanuni za usajili.
Mngereza alisema baada ya tathmini hiyo, baraza litarudi kwenye mwongozo wa awali wa mashindano hayo kwa utaratibu wa baraza kisha watatoa tamko, kwa sababu Lino Agency hawawezi kupewa kibali bila tathmini ya wadau.“Leo ndiyo tumefanya tathmini kusema kwamba majibu yatatoka leo au kesho ni vigumu sana, tunakaa chini tunaangalia, hiki siyo kitu pekee ambacho tunafuatilia, hawawezi kupewa kibali kabla ya tathmini,” alisema Mngereza.
Hatua zitachukuliwa
Hata hivyo, alisema Kamati ya Miss Tanzania kupitia kampuni yake ya Lino Agency, imekiuka kanuni na utaratibu wa mashindano hayo na hivyo itachukuliwa hatua.
“Tukirudi katika kanuni kuna vitu vingi sana ambavyo wamekiuka kimojawapo ni kutetea yale ambayo yalitolewa majibu yasiyo sahihi, kwamba kamati nzima hatimaye ikasema kwamba hiki cheti walichotuletea ni sahihi, sasa ninajiuliza wewe unawezaje kusema cheti ni sahihi huku hujathibitisha,” alisema na kuongeza:
“Ndicho kilichojitokeza katika tathmini, alitakiwa kuwasiliana na mamlaka husika, kama ni mtihani kuna Necta na kama cheti cha kuzaliwa kuna Rita, kwa hiyo wasingengoja wadau wapige kelele, waandishi wa habari wamkalie kooni kwa kulisimamia hili ndipo utekelezaji ufanyike,” alisema.
Mngereza aliongeza kuwa hilo ni kosa mojawapo na mwaka huu wamekiuka sheria, kwa hiyo Wizara na Basata itatoa tamko kuhusu mashindano hayo.
“Tutakuja na majibu ya tamko la Basata kwa niaba ya Serikali, pia ile kauli kuwa wizara iunde kamati ya kufuatilia si sahihi, hakuna mahali ambako kisheria wizara inaweza kuunda kamati, yeye ndiye mwenye miongozo, hivyo anatakiwa awajibike kupitia miongozo yake, tathmini ni sehemu ya maoni ya wadau mambo ambayo yanapaswa kubadilika,” alisema Mngereza.
Naye Mkurugenzi wa Lino Agency, Hashim Lundenga alisema suala lililojitokeza mwaka huu lilikuwa nje ya uwezo wao, kwani cheti kilikuwa ni halisi kutoka Rita na ndiyo maana walimwamini Sitti, lakini warembo wengi wamekuwa wakidanganya umri.
No comments:
Post a Comment