Friday, 21 November 2014
MLINZI AGEUKA KUWA NESI KIGOMA
KITUO cha Afya Nguruka wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma kinakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi hali iliyofanya mlinzi wa usiku katika kituo hicho, Boaz Selelo Kiganamo kutumika kama mtoa huduma katika kliniki ya baba, mama na mtoto.
Hali hiyo inatokana na ongezeko kubwa la akinamama wajawazito wanaohudhuria kliniki sambamba na kuwahi kituo cha afya wakati wa kujifungua ikiwa ni matokeo ya kampeni inayojulikana kama Thamini uhai okoa maisha ya mama na mtoto inayoendeshwa na Shirika la World Lung Foundation.
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Nguruka, Staford Chamgeni amekiri kuwepo ongezeko kubwa la akinamama wajawazito na watoto wanaohudhuria kwenye kituo na kubainisha kwamba ongezeko halilingani na ikama ya watumishi waliopo.
“Kwa kweli kwa sasa idadi ya kina mama wajawazito ni kubwa na hiyo imefanya tukabiliwe na mzigo mzito wa kuwahudumia na ndiyo maana hata watumishi wa idara nyingine wanalazimika kufanya kazi ya kusaidia katika Idara ya Kliniki,” alisema Mganga huyo Mfawidhi.
Akizungumzia hali hiyo mlinzi huyo alisema kuwa baada ya kumaliza zamu yake ya ulinzi usiku analazimika kusaidia kufanya kazi kwenye kliniki ya baba, mama na mtoto kutokana na upungufu mkubwa wa watumishi uliopo kwani wahudumu waliopo wame kuwa wakikabiliwa na mzigo mkubwa wa watu wanaofika kupata huduma kituoni hapo.
Kwa upande wake Maria Josephat, Muuguzi katika Kituo cha Afya Nguruka alisema kuwa ongezeko kubwa la akinamama wajawazito wanaofika kituoni hapo kupata huduma limewalazimu kufanya kazi masaa mengi ili kuendana na hali hiyo.
Hata hivyo alisema kuwa licha ya hali hiyo wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la kutopata malipo yao ya kufanya kazi saa za ziada kwa wakati na pengine kutopata kabisa na kwamba pamoja na hilo hawajakata tamaa katika kuwahudumia akinamama hao.
Kwa sasa kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa kituoni hapo zinaonesha kuwa zaidi ya akinamama wajawazito 200 hufika kujifungua kituoni hapo kwa mwezi kuanzia Septemba mwaka huu kutoka akinamama kati ya 80 na 130 waliokuwa wakijifungua kwa mwezi kabla ya zoezi hilo la uhamasishaji.
Akieleza mafanikio yaliyopatikana kutokana na kampeni hiyo, Anna Zakaria, Muuguzi Mkunga katika chumba cha upasuaji kituoni hapo alisema kuwa kufuatia kampeni hiyo kumekuwa na mafanikio katika kupunguza idadi ya akinamama wanaojifungua kwa njia ya upasuaji kutoka akinamama saba hadi 10 na kufikia akinamama 3 hadi 5.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Albert Mumwi amekiri kuwepo kwa upungufu mkubwa wa watumishi kwenye vituo vya utoaji huduma na kwamba kwa sasa kliniki za baba, mama na mtoto zimekuwa na ongezeko kubwa ambalo haliendani na idadi ya watumishi waliopo.
Mumwi alisema kuwa kutokana na hali hiyo Halmashauri imekuwa ikitoa posho ya kufanya kazi saa za ziada ingawa bado hata kiasi
kinachotengwa hakitoshelezi idadi ya watoa huduma wanaopaswa kulipwa.
CHANZO: HABARI LEO
FUATILIA JINSI SAKATA LA TEGETA ESCROW ACCOUNT LILIVYOTIKISA BUNGE JANA
WABUNGE jana waliungana bila kujali vyama vyao, kutetea kuwasilishwa bungeni na kujadiliwa kwa ripoti ya sakata la uchotaji fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow baada ya kuwapo kwa taarifa kuwa Mahakama imezuia.
Katika kile kilichoonekana kuwa wabunge wanataka mbivu na mbichi za sakata hilo ziwekwe hadharani, walisema hatua yoyote ya kuzuia suala hilo lisijadiliwe, inaweza kulivuruga Taifa na wao kulaumiwa.
Hata hivyo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitoa angalizo kuwa ni vyema kuwapo kwa utulivu na kila mhimili kusimamia mamlaka yake, na busara kutumika.
Bunge liliingia katika mjadala baada ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), kuomba ufafanuzi kutokana na kauli ya Waziri Mkuu wakati wa kipindi cha Maswali ya Papo kwa Hapo.
Akijibu swali la Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde (Chadema), Waziri Mkuu Pinda alisema yeye kama Mwanasheria ingawa si Mwanasheria Mkuu, kuna kesi zaidi ya 10 mahakamani kuhusu hilo, hivyo si vyema kuanza mjadala utakaotibua suala hilo.
Alisema hiyo si mara ya kwanza kwa Bunge kutoshughulika na suala linaloendelea mahakamani.
Kauli hiyo ndiyo iliyomsimamisha Kafulila na wabunge wengine wawili, Esther Bulaya (Viti Maalumu – CCM) na Moses Machali (Kasulu Mjini – NCCR- Mageuzi), huku Kafulila akitaka uhakika wa kauli ya Waziri Mkuu kama ripoti hiyo itapelekwa bungeni kujadiliwa au la.
Kutokana na hali hiyo, Naibu Spika alitoa fursa kwa wabunge kadhaa kulijadili suala hilo kwa nia ya kumsaidia kufikia maamuzi, lakini wote waliosimama ukiondoa Waziri Mkuu, walitaka ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), iwasilishwe bungeni na ijadiliwe.
Kwa sasa, ripoti hiyo inafanyiwa uchambuzi kwa njia ya uchunguzi na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) chini ya Kabwe Zitto, kabla ya kuwasilishwa bungeni.
Wa kwanza kumshauri Naibu Spika alikuwa Kafulila aliyesema kuwa suala hilo ni mtihani kwa Bunge, na ili nchi isiingie katika machafuko, ripoti hiyo haina budi kuwasilishwa ndani ya Bunge.
“Bunge ndicho chombo chenye mamlaka ya mwisho katika nchi, watu watatupima kama tunatosha kuisimamia Serikali kwa jinsi tutakavyoshughulikia suala hili. Bunge lazima liheshimiwe, hatuwezi kuwalinda watu wachache. Hiki ni kipimo cha uhalali wetu,” alisema.
Bulaya alisema Bunge lazima liheshimiwe, na kwamba “CCM haiwezi kukubali kuchafuliwa na watu wachache, kila mtu ale kwa urefu wa kamba yake. Ujangili, dawa za kulevya, Escrow marufuku.”
Naye Mbunge wa Longido, Michael Laizer (CCM), licha ya kukiri kuwa miongoni mwa wasiolifahamu vyema suala hilo, lakini alisema ni busara likajadiliwa na Bunge.
“Mimi silielewi vizuri, lakini ni jambo kubwa linaloumiza vichwa. Kuna minong’ono mingi, kuna orodha inatajwa ya wezi, hawajulikani ni kina nani, wengine wamo humo ndani. Naibu Spika tusifiche wezi, kila kitu kiwekwe waziwazi, tuelewe, wengine wanapiga siasa. Ije ripoti haraka, waliokula tuwaseme, halitupi raha,” alisema Laizer.
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), alisema ni vyema ripoti ikawasilishwa ili kujua mwizi ni nani na kila mtu abebe msalaba wake.
“Huu ndio wasaa wa ukweli, wasaa wa uamuzi. Hapa kuna watu waliitana tumbili na mwingine mwizi. Sasa ni wakati mwafaka kujua mwizi ni nani na tumbili ni nani,” alisema Msigwa.
Naye James Lembeli wa Jimbo la Kahama (CCM), alisema kama Operesheni Tokomeza ilikwenda na baadhi ya mawaziri, kuna kigugumizi gani katika Escrow.
“Kila mtu atahukumiwa kwa matendo yake, kama ni mtego basi uteguliwe. Historia itakukumbuka Naibu Spika kwa jinsi utakavyoshughulikia suala hili,” alisema.
Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR- Mageuzi), alisema lazima kuwapo na uadilifu na uaminifu, hivyo waliohusika na sakata hilo waende na maji, nchi itulie.
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), akizungumza kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, alisema Mahakama haiwezi kulifundisha kazi Bunge wala kulielekeza nini cha kufanya kwani haina mamlaka hayo.
“Kama Bunge la Tisa linakumbukwa kwa jinsi lilivyoshughulika na suala la Richmond, Bunge hili litakumbukwa kwa suala hili la Escrow. Ripoti iletwe hapa, wa kusuka na kunyoa tumjue,” alisema Lissu.
Akizungumzia maendeleo ya kazi yao, Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, alisema wako tayari kuiwasilisha ripoti yao bungeni.
“Sisi hata kesho (leo) tunaweza kuiwasilisha bungeni. Jana tumewahoji CAG, Takukuru na TRA na wamemaliza kazi yetu. Rasimu ya kwanza inaandaliwa leo (jana) na kesho inaweza kuingia bungeni, tukalijadili hili ili liishe,” alisema Zitto.
Hata hivyo, Waziri Mkuu Pinda alisema si kazi ya Mahakama kuficha uozo, lakini ni muhimu kila mhimili wa Dola ukatenda mambo kwa mujibu wa Katiba.
“Hata mimi nataka yajadiliwe yaishe, lakini tutumie busara kubwa ili kuondoa mwingiliano na chombo kingine cha maamuzi kama inavyotakiwa,” alisema.
Akihitimisha mjadala wake, Naibu Spika Ndugai alifanya rejeo la kauli ya aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta akisema; “tukiwa viongozi hatuwezi kutengeneza umoja katika uozo.” Ndugai alisema kwa kutazama hali ya wabunge ilivyokuwa jana wakati wa kumshauri, aliahidi kuwa “tutatenda haki katika jambo hili.”
CHANZO: HABARI LEO
WAZAZI MISS TANZANIA WADAI CHAO MAPEMAAAAAA
Wazazi wa Miss Tanzania mpya, Lilian Kamazima wameitaka Kamati ya Miss Tanzania iwape maelezo ya uhakika kuhusu zawadi na taji la binti yao kwa kuwa hadi sasa wako njiapanda.
Kauli hiyo ya Eva na Deus Kamazima imekuja siku chache baada ya mrembo huyo kuwasili jijini Arusha akitokea Dar es Salaam.
Wakizungumza nyumbani kwao, Majengo Juu jijini Arusha wazazi hao walionyeshwa kushangazwa na hatua ya kumpokea binti yao akiwa hana taji, pamoja na fedha ambazo alistahili kupatiwa kama mshindi.
Walisema kuwa walimpokea binti yao kama ‘yatima’, hata tiketi ya ndege alilazimika kulipiwa na Mkurugenzi wa Kampuni ya Mwandago Investment Ltd, aliyemuibua katika ngazi ya Kanda ya Kaskazini.
“Tunaiomba Kamati ya Miss Tanzania itupe maelezo ya kina kuhusu zawadi, taji pamoja na vitu vingine kwa kuwa tumempokea binti yetu kama yatima bila zawadi wala taji,” walieleza wazazi hao kwa nyakati tofauti.
Awali, mrembo huyo alisema kuwa pamoja na kwamba bado hajakabidhiwa taji wala zawadi yoyote na Kamati ya Miss Tanzania, lakini kitendo cha kupewa kiti hicho ameridhika.
“Sijapewa taji wala zawadi , lakini kitendo cha kupewa kiti cha umalkia nimeridhika,” alisema Lilian.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino International Agency, Hashim Lundenga alipoulizwa kuhusu madai hayo alisema kuwa ni kweli bado hawajamkabidhi fedha na zawadi kwa kuwa kuna taratibu za kiofisi bado zinafanyika.
“Ni kweli, tulimwambia atuachie akaunti yake kwa kuwa kuna taratibu zinafanyika, tutamwekea pesa na kuhusu zawadi huyo alirithi taji, hakuwa mshindi wa kwanza, lazima mwelewe,” alisema Lundega.
PUTIN: MAREKANI NA WAPAMBE WAKE WAMECHEMKA
Rais Vladimir Putin wa Russia amesema kuwa juhudi za Marekani za kutaka kuipigisha magoti nchi yake zimegonga mwamba. Rais Putin amesema kuwa vikwazo vilivyowekwa na Marekani na waitifaki wake dhidi ya Russia ni fursa kwa ajili ya ustawi wa nchi hiyo. Putin amesema kuwa, nchi zilizoiwekea Russia vikwazo zina matatizo mbalimbali na kwamba zimepoteza masoko ya bidhaa za chakula na za kilimo ya Russia. Ameongeza kuwa na hapa ninamkuu" sisi tumestafidi na miamala mibaya ya washirika wetu na nchi ambazo zilikuwa zimepata nafasi katika masoko ya bidhaa za chakula na kilimo za Russia na tumeziwekea vikwazo nchi hizo" mwisho wa kunukuu.
Rais wa Russia amesisitiza pia juu ya udharura wa kustafidi na sekta za kiuchumi za Russia zinazotokana na fursa zilizopotea kutokana na vikwazo vya nchi za Magharibi na Moscow kujibu vikwazo hivyo sambamba na kuboresha uwezo wake katika nyanja mbalimbali za nchi hiyo.
UN YATAKA MFĂ€NYAKAZI WAKE KUACHIWA HURU
Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kuachiwa huru mfanyakazi wake aliyetekwa nyara na kupelekwa kusikojulikana nchini Sudan Kusini.
Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) linalowasaidia maelfu ya raia walioathiriwa na vita kwa kipindi cha karibu mwaka mmoja sasa huko Sudan Kusini limetangaza kuwa, lina wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya Mark Diang ambaye alitekwa nyara na genge la watu waliokuwa na silaha Oktoba 16 katika uwanja wa ndege wa mji wa Malakal. Mkuu wa WFP nchini Sudan Kusini, Joyce Luma amesema, kutekwa nyara na kutoweka kwa Mark Diang kumekuwa na taathira mbaya kwa wafanyakazi wenzake ambao sasa baadhi yao wanashindwa kufanya kazi kwa kuhofia maisha yao.
Wafanyakazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa wamekuwa wakitekwa nyara au kuuawa mara kwa mara katika nchi iliyokumbwa na vita vya ndani ya Sudan Kusini. Mwezi Agosti mwaka huu pekee watu waliokuwa na silaha walishambulia na kuwaua wafanyakazi wasiopungua 6 wa Umoja wa Mataifa nchini humo.
BOKO HARAM YAUA 45 NIGERIA
Shambulizi linalodhaniwa kuwa la wapiganaji wa kundi la kitakfiri la Boko Haram limeua watu wasiopungua 45 huko kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Shambulizi hilo limefanyika katika kijiji cha Azaya Kura katika eneo la Mafa kwenye jimbo la Borno na baadhi ya walioshuhudia tukio hilo wanasema idadi ya watu waliouawa huwenda ikaongezeka kutokana na majeruhi wengi wa shambulizi hilo.
Kaimu wa Gavana wa jimbo hilo Shettima Lawan ameiomba serikali kuu ya Nigeria kuchukua hatua za haraka za kuwaokoa watu wa eneo hilo.
Shambulizi hilo limefanyika siku chache baada ya Waziri wa Sheria wa Nigeria Mohammed Adoke kusema kuwa, Rais Goodluck Jonathan wa nchi hiyo anatarajiwa kuliomba Bunge lirefushe muda wa hali ya hatari katika majimbo ya Yobe, Borno na Adamawa kutokana na machafuko yanayosababishwa na kundi la Boko haram.
Kundi hilo linahusika na mashambulizi na mauaji mengi yanayofanyika katika maeneo hayo ya kaskazini mwa Nigeria.
HALI MBAYA YA KIBINADAM YANUKIA LIBYA
Kamisheni ya taifa ya kutetea haki za binadamu nchini Libya imetahadharisha juu ya uwezekano wa kuzuka hali mbaya ya kibinadamu katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Taarifa ya kamisheni hiyo imesema kuwa, kutokana na kushitadi ghasia na machafuko, idadi ya wakimbizi wa ndani na nje ya nchi inazidi kuongezeka kila uchao; jambo linaloweza kusababisha kuibuka hali mbaya ya kibinadamu. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, tayari idadi ya wakimbizi kwenye kambi za ndani ya nchi imeongezeka katika hali ambayo huduma muhimu kama vile maji na vyoo ni adimu.
Mapigano kati ya jeshi la serikali na makundi ya wanamgambo wenye silaha nchini Libya hadi sasa yamesababisha zaidi ya watu nusu milioni kukimbia makazi yao na kuwa wakimbizi ndani ya nchi huku wengine wengi wakikimbilia nchi jirani za Misri na Tunisia kutafuta hifadhi.
WAASI WA KUSINI MWA SUDAN WATAKA KUJITAWALA
Waasi wa Sudan wanataka majimbo mawili yaliyogubikwa na machafuko huko kusini mwa nchi hiyo ya Kordofan Kusini na Blue Nile yapewe mamlaka ya ndani ya kujitawala. Hayo yameelezwa na Yasir Arman mkuu wa jopo la waasi kwenye mazungumzo ya amani na serikali ya Sudan. Arman ameelezea sababu kuu ya kutaka kupewa mamlaka ya ndani kwa kusema kuwa, majimbo hayo yanakaliwa na idadi kubwa ya Wakristo, hivyo mila na utamaduni wa wakazi wa majimbo hayo inatofautiana mno na wakazi wa majimbo mengine ya Sudan. Yasir Arman ameongeza kuwa, wakazi wa maeneo ya Darfur, eneo la mashariki mwa Sudan na jimbo la al Jazira wana haki pia ya kuwa na mamlaka ya ndani ya kujitawala, ili waweze kuendesha mambo yao kwa uhuru zaidi. Inafaa kuashiria hapa kuwa, Sudan Kusini ambayo kabla ya kujipatia uhuru ilikuwa ikijulikana kama kusini mwa Sudan, mwaka 2011 ilitangaza kujipatia uhuru wake baada ya kufanyika kura ya maoni ya kuainisha mustakbali wa eneo hilo lenye majimbo kumi. Licha ya Sudan Kusini kujipatia uhuru lakini nchi hiyo bado inashuhudia machafuko na mapigano ya ndani.
Subscribe to:
Posts (Atom)