Watu sita wa familia moja akiwamo Kapteni mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ), wamekufa papo hapo baada ya kuteketezwa kwa moto jijini Dar es Salaam.
Janga hilo la moto limetokea jana saa 10:30 alfajiri katika eneo la Kipunguni A, Ukonga Banana, wilayani Ilala.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki alisema kuwa moto huo ulizuka ghafla katika nyumba inayomilikiwa na mstaafu huyo wa Jeshi, David Mpira anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 55 na 60.
Alisema wengine waliokufa katika ajali hiyo ni mke wa marehemu, Selina Yegela anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 50 na 55, ambaye pia ni mstaafu wa iliyokuwa Kampuni ya Kuhudumia Ndege (DAHACO), sasa Swissport.
Aidha, moto huo pia umesababisha vifo vya watoto wawili wanaokadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 20 na 30 ambao ni, Lucas Mpira na Samwel Yegela.
Kamanda Nzuki alisema wajukuu wa marehemu nao wamekufa katika ajali hiyo, ambao ni Selina Emmanuel (9) mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Minazi Mirefu na Pauline Emmanuel (3), mwanafunzi wa chekechea katika Shule ya Tumaini iliyopo Kitunda.
“Chanzo cha moto huo bado hakijafahamika, tunaendelea na uchunguzi na tunashirikiana na Shirika la Umeme (Tanesco) ili kubaini chanzo kilichosababisha moto huo,” alisema Nzuki.
Maiti wamehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na uchunguzi bado unaendelea.
No comments:
Post a Comment