Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Prof. Sospeter Muhongo akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano aliouitisha jana ofisini kwake, ametangaza kujiuzulu wadhifa wake wa Uwaziri baada ya kutuhumiwa kuwa yeye ndiye tatizo linaloendeleza malumbano baina ya Serikali na Bunge kuhusu fedha za akaunti ya Tegera Escrow.
“Nimejiuzulu bila kushinikizwa na mtu yeyote. Mimi ndiyo nitamaliza mjadala huu wa sakata la escrow, nchi ina mambo mengi ya kitaifa yanayotakiwa kujadiliwa lakini watu wamekazana na escrow.
"Nimemuandikia Rais barua rasmi ya kujiuzulu wadhifa wangu. Nimemuomba rais kuachia ngazi ili niipe nafasi serikali yangu kufanya kazi... Nitaendelea kuwa mbunge na mshauri.
“Sidhani kwamba cheo cha mtu mmoja cha uwaziri ni muhimu kuliko hawa masikini ambao wanateseka mchana na usiku.Kwa hiyo nimesema ni sehemu ya suluhisho.
“Nimemuomba Mheshiwa Rais kwamba tafadhali naomba niachane na nafasi ya Uwaziri kusudi taifa lisengo mbele.Hakuna sababu ya kuendelea kulumbana, tunapoteza muda na mali zetu, tunapoteza nguvu zetu wakati ambapo malumbano hayana mwisho” alisema Profesa Muhongo.
Kujiuzulu kwake kumetokana na shutuma zilizomwandama za jinsi alivyoshughulikia suala hilo na Wizara yake ikiwa ni pamoja na uchowaji wa fedha kiasi cha shilingi bilioni 306/= kutoka kwenye akaunti hiyo.
Prof. Muhongo amezidi kusisitiza kuwa yeye hakuhusika na chochote kile katika hilo: "Sikuwahi kuchukua rushwa na sihongeki... Mimi nashangaa leo watu kila kona wananiona mimi ni mwizi, yaani kama mimi ndiyo nimechukua mabilioni ya escrow wakati ukweli upo wazi.
"Wakati Wizara ya Nisharti inaingia kwenye mkataba huo mimi sikuwepo kwenye nafasi ya Uwaziri, lakini leo watu bado wananiona mimi ni mwizi.
"Acha niaachie ngazi nafasi hii ya uwaziri kwani imekuwa ni shida sana, mimi ni mtu msomi nimepata tuzo sehemu mbalimbali duniani, nasifika kwa kutoa ushahuri wenye tija, lakini leo naonekana mwizi, wakati historia yangu inaonesha mimi ni mtu msafi sina doa na wala sijawai hata kumwibia mtu, lakini watu wananiona mimi mwizi” , Alisema Muhongo na kuendelea kueleza kuwa, baada ya kutafakari sana aligundua kwamba amenyooshewa kidole yeye binfasi, ni kwa sababu hiyo ameamua kujiuzulu kwa kuzitaja sababu mbili, kuwa:-
Ana matumaini kuwa kuachia kwake ngazi, mjadala wa ‘escrow’ utakuwa umefikia tamati.
Anafanya hivyo ili kukiweka safi Chama Cha Mapinduzi ambacho kimekuwa kinanyooshewa kidole.
"Uamuzi huu nimeufanya kwa sababu zifuatazo kwanza nataka Serikali ibaki kushughulikia matatizo ya wananchi badala ya Serikali kukaa inashughulikia suala la Escrow.
"Ninaachia ngazi za Uwaziri kwa sababu ninataka kamati za CCM ziendelee kutatua kero za wananchi kuliko kukaa kwenye vikao masaa mengi wanazungumzia masuala ya Escrow.
"Vilevile naachia ngazi kwa sababu kule Bungeni mimi nataka niwe mbunge wa kawaida, na si ubunge wa kawaida tu lakini nafasi ya Uwaziri nitawaachia wengine. Hii nayo itatoa fursa kwa bunge letu kutumia muda wake vizuri na rasilimali zake vizuri kwa manufaa ya wananchi.
"Naachia nafasi hii kwa sababu Watanzania wamechoka, Escrow haina tija kuijadili kila siku asubuhi mapaka jioni badala ya umasikini wao, hebu tuwaachie wananchi kuliko kuendelea na malumbano yasiyokuwa na mwisho."
Amesema kwa namna moja ama nyingine, sakata hilo si tu kuwa limekuwa likikigharimu Chama bali pia baada ya kutafakari aliwasiliana na mkuu wake wa kazi, Rais Jakaya Kikwete na familia yake na watu wake wa karibu kuwataarifu kuwa anajiuzulu.
Muhongo amesema kuwa sakata hilo lilitawaliwa na mambo makuu manne:-
Mvutano wa kibiashara
Mvutano wa kisiasa
Mvutano wa uongozi na madaraka
Ubinafsi.
Amesema akiwa katika nafasi hiyo, aliweza kufanya mengi ikiwa ni pamoja na kuwapeleka vijana wengi nje kusomea masuala ya gesi, nishati na sayansi kwa ujumla kwani ili Taifa liendelee, linahitaji kuwa na wataalamu katika sekta hiyo muhimu.
“Nimeshirikiana na Makamu wa Rais, nimeshirikiana na Waziri Mkuu na kusaidia kuwaletea wananchi maendeleo hadi leo tukaweza kusimama na kusema asilimia 40 ya Watanzania wanatumia umeme”
Alilishukuru Baraza la Mawaziri, Bunge, Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kwa ushirikiana wao walioutoa kwake na kueleza kuwa yeye daima atawatumikia wananchi.
Waziri Muhongo aliteuliwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini mwezi Mei mwaka 2012 baada ya kuteuliwa kuwa mbunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Profesa Jakaya Kikwete.
Muhongo anakuwa mtumishi wa tatu kuachia nafasi yake kutokana na kuhusishwa na sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow, baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Fredrick Werema kujiuzulu wadhifa huo huku Rais akitangaza kumvua Uwaziri Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka. Pia baadhi ya watumishi wa Serikali kutoka taasisi mbalimbali wakifikishwa mahakamani kutokana na tuhuma zinazohusishwa na sakata hilo.
Ameahidi kuwaeleza Watanzania ukweli wa sakata la akaunti ya Tegeta Escrow na kujiuzuru kwake ili kuvunja majungu yanayoendelea kuitesa Tanzania na watu wake.
No comments:
Post a Comment