Sunday 25 January 2015

MREMBO MTANZANIA ALIYEJIUNGA NA FREEMASON AJITOKEZA AELEZA MAZITO

  
Happiness Wilfred Nassari (27), ameibuka na kudai kuwa amekuwa akisali bila nguo kwenye ibada ya imani ya Freemason inayosifika kwa ushirikina. 

Katika mahojiano yaliyofanyika hivi karibuni Bamaga, Mwenge jijini Dar, Happiness alisema kuwa, alianza kuingia kwenye imani hiyo kwa kwa kupitia kaka yake mmoja (jina tunalo) ambaye ni tajiri wa kupindukia kutokana na kuwa mshiriki wa Freemason.

“Nilipojiunga ilikuwa si kwa matakwa yangu, kwani nilianza kwa kupata matatizo ya kuumwa magonjwa ya ajabuajabu, ikiwemo kutokwa na wadudu usoni kiasi cha kunitoa vidonda,” alisema mrembo huyo huku akionesha makovu ya vidonda hivyo.

“Hali ilipokuwa mbaya, ilibidi niende kwa mganga mmoja wa kienyeji ambaye aliniambia nimetupiwa majini ya kunuka ambayo yanabadilika harufu kila mara, lakini alitaka nimlipe shilingi milioni 5 ili anitibie, nikashindwa, nikaondoka.

“Kuna wakati vile vidonda vilisababisha nianze kufuatwa na nzi wengi hadi watu wengine wakawa wanadai kusikia harufu, ndipo nikaenda kwenye Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Arusha  kwa Mchungaji Olduvic kuombewa ndipo nzi wakatoweka na harufu kupungua,” alisema
Alisema baadaye alijikuta akiwa muumini mkubwa wa Freemason lakini si kwa hiari yake. Akaongeza kuwa, alipewa uwezo wa kusafiri mbali ya Tanzania kwa usiku mmoja na kukutana na wazungu ambao anaamini wana uwezo mkubwa wa mambo ya kiroho kuliko walokole wa siku hizi.
“Hali hiyo ilifika mahali mpaka nikaanza kushirikishwa ibada zao kwa kusali bila nguo. Tulikuwa tunakwenda kwenye hekalu la ibada tukiwa tumevaa lakini tukifika ndani tunavua nguo na kubaki kama tulivyozaliwa na kuanza kusali. Hekalu hilo lipo hapahapa Dar es Salaam, lakini naomba nisiseme lilipo.

“Jambo kubwa ambalo nataka kulisema kwa leo, si kwamba nimeachana nao, bado nipo. Ila nimejikuta nikiwa sina amani kwa kuficha habari hizi.“Ninachojua hata hapa ninapozungumza na nyinyi wanajua kila kitu, kwani wananifuatilia bado kwa sababu walishanipa fedha kwa ajili ya mtaji wa biashara, lakini kusema ukweli sina amani,” alisema Happiness na kuanza kulia.

Alimalizia kwa kuweka wazi kwamba, kwa wale wanaotafuta utajiri kwa kupitia imani ya Freemason, anawashauri kuachana na akili hiyo kwani utajiri wao unakuwa na masharti mengi ikiwemo kuua ndugu wakiwemo wazazi.

Credit:GPL


No comments: