Mfanyakazi wa kampuni ya mafuta ya Lake Oil, Deocres Deus Ruta (32) anayedai kunyanyanswa na mabosi zake.
Baadhi ya vigogo wa kampuni ya mafuta ya Lake Oil wanadaiwa kumvua nguo mfanyakazi wao Deocres Deus Ruta (32) (pichani)ambaye ni dereva wao pia vijana wawili ambao siyo wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Akizungumza katika ofisi za gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita Ruta alidai kwamba Desemba 11, mwaka huu waliingizwa katika ofisi moja iliyopo Makambako mkoani Njombe na kuwakuta mabaunsa wawili na mabosi wengine akiwemo aliyetoka katika ofisi zao za Kigamboni Dar, walipigwa na kipande cha chuma katika joiti zao za magoti.
“Wenzangu walikuwa wa kwanza kufika katika ofisi hiyo niliwakuta wamevuliwa nguo, nami nilipofika waliniambia nivue jaketi waliniadhibu kisha kunilazimisha nivue nguo zote, nilihisi wanataka kunifanyia kitendo kibaya, kwa ujasiri, nilifungua mlango na kukimbilia katika gari la mizigo nililokuwa nikiendesha lililobeba mzigo wa shaba nikitokea nchini Kongo (DR CONGO).
“Nilipofika katika gari nilitafuta kisu ili nijichome nife kuliko kudhalilishwa, walininyang’anya kila kitu changu ikiwemo simu, nguo za familia yangu nilizowanunulia kwa ajili ya sikukuu, paspoti na leseni ya udereva kisha tulipelekwa polisi Makambako.
Kamanda wa polisi mkoa wa Njombe SACP Flugence Ngonyani.
“Tuliwekwa ndani kwa siku tatu bila kuchukuliwa maelezo, lakini hapo mahabusu tulikaa siku sita ndipo tukadhaminiwa.“Walituweka ndani kwa madai kuwa tuliwaibia shaba, kitu ambacho si kweli ila wakati tulipokuwa tukitoka Kongo tulipofika maeneo ya Igawa, Makambako kwenye kilima, saa 1.30
usiku, tuliwaona vijana wanne waliovaa kininja wakiwa na mapanga, walidandia gari letu na kuanza kukata mikanda iliyofungia mzigo.
“Nilipoona gari linakuja mbele yangu nililizibia njia likasimama ndipo wale vijana wezi waliposhuka na kukimbilia porini.“Baada ya kuongea na yule tuliyezuia gari lake kuhusu wezi hao tulianza safari na kuwapigia simu mabosi wetu, walituambia tukatoe taarifa polisi,” alisema Ruta.
Aliongeza kuwa walifanya ukaguzi na kugundua kuwa kuna kipande cha shaba kimeibiwa.
Alidai walifikishwa polisi ili wasiweze kuwashitaki waliofanya unyama huo na hati ya matibabu (PF 3) walinyimwa.
“Mwandishi wa gazeti hili alimtafuta kwa njia ya simu Mkurugenzi wa Lake Oil, Ally Edha Awadhi lakini hakupatikana lakini alipotumiwa ujumbe kuulizwa tukio hilo alijibu:
“Ripoti nilizopata ni kuwa huyo kijana aliiba na ripoti ipo Makambako polisi, sasa kama ameamua kunidhalilisha tutakutana mahakamani. Hakuna aliyepigwa huyo ni mwongo na anakabiliwa na kesi ila sasa anajaribu kupotosha ukweli.”
Kamanda wa polisi mkoa wa Njombe SACP Flugence Ngonyani alipoulizwa kwa njia ya simu alisema kwamba hana taarifa hizo na aliahidi kuzifuatilia.
No comments:
Post a Comment