Sunday, 28 December 2014
ALIYEKUWA KATIBU MKUU WA YANGA ATAFUTWA NA POLISI KWA TUHUMA ZA UBADHILIFU
JESHI la Polisi jijini Dar es Salaam limekuwa likiendelea kumsaka aliyekuwa Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu.
Habari za kipolisi kutoka ndani ya Jeshi hilo zimeeleza kwamba juhudi za kumtia nguvuni Njovu anayetuhumiwa na ubadhilifu zimekuwa zikiendelea kwa juhudi kubwa.
“Unajua askari wetu walikwenda kumshika Njovu wakiongozana na mwanasheria wa Yanga, lakini akashitukia mtego na kutimua mbio. Sasa juhudi zinafanyika ili kumshika kwa kuwa tuna RB yake.“Lengo ni kumtia nguvuni ili aweze kujibu mashitaka yanayomkabili kuhusiana na ubadhirifu,” alisema mtoa habari ambaye hakutaka kuandikwa gazetini kwa madai yeye si msemaji wa jeshi hilo.kwa upande wa Yanga, Mkurugenzi wa Habari, Jerry Muro alisema wanajua Jeshi la Polisi ndilo linahusika na suala la ufuatilia.
“Sasa kama liko mikononi mwa polisi, basi tuwaachie wao, nafikiri haitakuwa vizuri sisi tukawa wasemaji tena. Watakapokamilisha mambo yao kwa kufuata taratibu zao, huenda wakaeleza kinachoendelea,” alisema.
Tayari Mhazini wa Yanga aliishashikiliwa na jeshi hilo kabla ya kuachiwa kwa dhamana katika tuhuma zinazohusiana na jambo hilo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment