Wednesday 26 November 2014

SASA NI ZAMU YA WAKAZI WA BAGAMOYO KUPONDA MARAHA BAHARINI


“Kivuko hiki ndicho bora kuliko vyote kati ya 27 tulivyonavyo nchi nzima. Kitabeba watu zaidi ya 500 ukijumlisha na wengine watakaokuwa wamesimama”

Usafiri wa majini una raha yake, hasa ikiwa chombo unachotumia ni imara na chenye usalama usiotiliwa shaka.

Wasafiri kati ya Dar es Salaam na Zanzibar ni mashuhuda wa baadhi ya vyombo vya majini vyenye mvuto wa aina yake. Ukiwa katika vyombo hivi utafurahia mwonekano wake, mwendo na sifa nyinginezo.

Kwa watu wengi hasa wanaotumia vyombo hivi, usafiri katika maeneo hayo ni zaidi ya safari. Ni utalii wa aina yake.

Ukiondoa raha ya wasafiri wa Dar es Salaam na Zanzibar, sasa ni zamu ya wakazi wa Dar es Salaam na Bagamoyo. Kwa wasiotaka usafiri wa barabara, Serikali imewaletea usafiri wa majini. Kivuko cha Mv Dar es Salaam, kimewasili nchini tayari kutoa huduma ya usafiri kati ya maeneo hayo.

Pamoja na kivuko hicho kuelezwa kuwa kitasaidia kupunguza msongamano wa magari, matumizi yake yanaweza pia kuchukua sura ya utalii

“Hiki kivuko kitakuwa na matumizi mengi, wengine watapenda kufungia ndoa humo, wengine watakuwa wakitalii. Naomba Watanzania wakitunze ili kidumu,” anasema Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.

Mv Dar es Salaam

Katika hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2013/14, Dk Magufuli alitaja miradi mbalimbali itakayosaidia kupunguza foleni katika jiji hili. Miongoni mwa miradi hiyo ilikuwa ni ujenzi wa kivuko kitakachofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo.

Novemba 17, mwaka huu kivuko hicho kiliwasili nchini kutoka Bangladesh baada ya safari ya siku 14 kikiwa chini ya usimamizi wa mkandarasi, Kampuni ya Johs Graham-Hanssen M/S ya Denmark.

Dk Magufuli anasema kivuko hicho chenye thamani ya Sh7.9 bilioni, kina mwendo wa kasi zaidi kuliko kivuko chochote nchini na kina uwezo wa kubeba watu 300 waliokaa, huku wengine wakisimama.

Anasema kivuko hicho pamoja na miradi mingine kama vile ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka (BRT), barabara za pembeni na barabara za juu, kitasaidia kupunguza msongamano wa magari ambao umekuwa sugu kwa sasa.
Chanzo: Mwananchi

PAPA FRANCIS ATAKA MAJADILIANO NA WAPIGANAJI WA DOLA YA KIISLAM


Baba mtakatifu Francis ametaka milango ya majadiliano na kundi la wanamgambo wa dola ya kiislam iwe wazi ,ingawa hali ni mbaya na ya kutatiza katika maeneo wanako tekeleza mashambulio yao.

Papa Francis ameyasema hayo wakati akirejea mjini Rome, Italia,baada ya kulitembelea bunge la muungano wa jumuiya ya Ulaya lilifanyika katika mji wa Strasbourg, Papa pia amesisitiza makubaliano ya kimataifa kutokomeza ugaidi yalikuwa muhimu.na hakuna ulazima wa nchi kupigana na ugaidi ikiwa peke yake nguvu ya pamoja ni muhimu sana.

Akilihutubia bunge hilo ,alishusha mvua za lawama kwa muungano huo kuwa una hatia kwa kuweka sheria zilizokuwa kali na za kuumiza, hasa katika suala la wahamiaji na kuonya kuwa Mediterranean isifanywe kuwa kaburi la wahamiaji wanaosafiri kwa boti kutokea upande wa kaskazini mwa Africa

UEFA: CHELSEA NOUUUUMAAAA....BAYERN YAGONGWA 3...


Usiku wa kuamkia leo kindumbwe ndumbwe cha michuano ya Klabu Bigwa barani Ulaya kiliendelea na kushuhudia Chelsea ikitoa kipigo cha mbwa mwizi mbele ya mashabiki wa Schalke 04 ya Ujuremani pale ilipoishindilia magoli 5 bila majibu.

Manchester City ya England nao wakawabamiza wababe wengine wa Ujerumani Bayern Munich kwa kwa kuwafunga magoli 3 - 2 na kufufua matumaini ya kusonga mbele katika michuano hiyo huku magoli yote matatu ya Man City yakitiwa kimiani Sergio Aguero.

Katika mechi nyingine Paris St. Germain ya Ufaransa waliwashikisha adabu Ajax ya Uholanzi kwa kuifunga magoli 3 - 1 huku Becelona kwa upande mwingine wakiisasambua Apoel Nicosia ya Syprus kwa kuishushia kichapo cha magoli 4 kwa yai.

CSKA Moscow ya Urusi na AC Roma zikatoka suluhu ya goli moja 1 - 1

Burudani hiyo itaendelea leo ambapo Liverpool ya England baada ya kufanya vibaya katika mechi zilizotangulia leo wanajaribu bahati yao wakiwa ugenini dhidi Ludogorets ya Bulgaria.

Arsenal nao watawakaribisha Borusia Dortmud ya Ujerumani huku vita vingine vikiwa ni kati ya FC Basel ya Uswis watakaopopepetana na Real Madrid. Malmo FF ya Sweden watakuwa wenyeji wa Juventus ya Italia

OBAMA AMPA POLE JK


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete mchana wa Jumatatu, Novemba 24, 2014 amepokea salamu za pole kutoka kwa Rais wa Marekani Mheshimiwa Barak Obama.

Katika salamu zake Rais Obama ameelezea kufurahishwa na taarifa kwamba Rais Kikwete anaendelea vyema kiafya baada ya kufanyiwa upasuaji kwa mafanikio na kuondoa tatizo la tezi dume alilokuwa nalo.

Rais Obama amesema katika salamu hizo kuwa alipata heshima kufanya ziara rasmi nchini Tanzania mwaka 2013, na pia kumualika Rais Kikwete kwenye mkutano wa  Marekani na viongozi wa Afrika mwaka huu.

“Nakutakia kasi ya kupona kabisa na nataraji kuendelea kufanya kazi nawe katika masuala tuliyokubaliana ya kipaumbele”, amesema Rais Obama kwenye salamu zake hizo.

Rais Kikwete amekabidhiwa salamu hizo na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Mhe. Liberata Mulamula, aliyekuwa ameongozana na maafisa waandamizi wa ubalozi waliofika Baltimore kumjulia hali.

Mhe. Mulamula amesema salamu kutoka sehemu mbalimbali duniani zimekuwa zikimiminika ubalozini kwa njia mbalimbali.

Taratibu za matibabu za Mheshimiwa Rais Kikwete zilikamilika Jumatatu, Novemba 24, 2014 asubuhi baada ya  madaktari bingwa katika Hospitali ya Johns Hopkins iliyoko mjini Baltimore, Jimbo la Maryland, Marekani, kumfanyia  hatua ya mwisho ya tiba.

Rais Kikwete ameendelea kupumzika na kuangaliwa kwenye Hoteli Maalum inayohusiana na Hospitali ya Johns Hopkins kwa siku tatu kabla ya kuanza safari ya kurejea nyumbani.

Kama kila kitu kitakwenda kama ilivyopangwa na madaktari, Rais Kikwete anatarajiwa kurejea nyumbani Jumamosi, Novemba 29, 2014.

Rais Kikwete aliondoka nchini Alhamisi ya Novemba 6, 2014, kwenda kufanyiwa uchunguzi wa afya yake lakini madaktari katika Hospitali ya Johns Hopkins waliamua kumfanyia upasuaji wa tezi dume Jumamosi ya Novemba 8, 2014.

Rais Kikwete anaendelea kuwashukuru Watanzania kwa sala na maombi yao ya kumtakia heri ya kupona haraka na kurejesha afya njema katika kipindi chote cha ugonjwa wake.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu – Dar es Salaam.

25 Novemba,2014

BOKO HARAM WAENDELEA KUFANYA YAO....SASA WATEKA MJI MWINGINEMWINGINE WA KASKAZIN

Duru za habari nchini Nigeria, zimetangaza kuwa, wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri wa Boko Haram wameudhibiti mji mwengine wa kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Hayo yamethibitishwa leo na kiongozi mmoja wa serikali katika bunge la seneti nchini Nigeria ambaye ni mkazi wa jimbo la Borno na kuongeza kuwa, wanachama wa kundi hilo lenye uelewa potofu kuhusu mafundisho ya Uislamu, wameudhibiti mji wa mpakani wa Damasak. Seneta huyo ameongeza kuwa, hivi sasa mji huo umetwaliwa na kundi hilo na kwamba, raia na askari wamelazimika kukimbia kuokoa maisha yao. Inaelezwa kuwa, awali wanamgambo wa kundi hilo waliokuwa wameficha silaha zao katika magari aina ya malori, walipeleka magari hayo katika soko la mji huo, na kuanza kuwamiminia risasi wafanyabiashara na raia wa kawaida, ambapo makumi ya watu waliuawa. Seneta huyo ameongeza kuwa, baada ya wanachama wa kundi hilo la Boko Haram kuudhibiti mji huo, walianza kubomoa na kuharibu nyumba nyingi ikiwemo hospitali na kwamba hadi sasa makumi ya wasichana na watoto wadogo wametekwa na magaidi hao.

TIGO TANZANIA YAGĂ€WA MABILIONI KWA WATEJA WAKE


Tigo imetangaza jana kwamba imetoa malipo yake ya kwanza ya kila robo mwaka ya kiasi cha shilingi bilioni 3 (dola milioni 1.8) kwa wateja wake wa Tigo Pesa. Mgao huu ni wa kwanza kati ya awamu nne za malipo zinazotarajiwa kufanyika kila mwaka.

Malipo haya yanafanyka miezi mitatu baada ya kampuni hiyo kulipa kiasi cha shilingi bilioni 14.25 (dola milioni 8.64) ambacho kilikuwa kimelimbikizwa katika mfuko wa fedha ya akaunti ya Tigo Pesa, malipo yaliyoifanya Tigo kuwa kampuni ya simu ya kwanza duniani kuwagawia faida watumiaji wake wa huduma ya fedha kwa simu za mkononi. Tigo Pesa ina jumla ya watumiaji milioni 3.6.

Meneja Mkuu wa Tigo Diego Gutierrez alisema, “Hii duru ya pili ya kutoa gawio ni udhihirisho tosha wa muendelezo wa kampuni yetu katika kuwanufaisha wateja na kuboresha maisha ya Watanzania. Malipo haya yanaenda kwa kila mtumiaji wa Tigo pesa wakiwemo mawakala wakuu, mawakala wa reja reja na watumiaji wa kawaida wa huduma hii. ”

“Gawio la kwanza lilikuwa kubwa zaidi kwa sababu faida ilimbikizwa kwa muda wa zaidi ya miaka mitatu na nusu ikilinganishwa na malipo haya ya pili ambayo yanatokana na malimbikizo ya faida ya fedha zilizohifadhiwa katika mifuko ya benki za kibiashara kwa muda wa miezi mitatu t kutoka Julai hadi Septemba 2014,” alisema Meneja Mkuu huyo.

Gutierrez alieleza kwamba, kama ilivyokuwa hapo awali, malipo wanayopata wateja awamu hii yanatokana na salio lao la kila siku kwenye akaunti zao za Tigo Pesa. Hii ni kwa wote; mawakala wakuu, mawakala wa reja reja na watumiaji wa kawaida.   

Mgao unaofuata wa mwezi Oktoba mpaka Desemba 2014 utalipwa mwezi Februari 2015.

Tuesday 25 November 2014

ALICHOKIANDIKA RAIS KIKWETE KUHUSU SKENDO YA KUWAHAMISHA WAMASAI LOLIONDO

‘Kumekuwa na taarifa katika vyombo vya habari na mitandaoni pia kwamba Serikali ilikuwa na mpango wa kuiondoa Jamii ya Wamasai katika eneo la Loliondo, ambapo Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu aliwahi kukanusha juu ya hilo siku tatu zilizopita.
Juzi kupitia ukurasa wa Twitter, Rais Kikwete ameandika kwamba Serikali haina mpango na wala haitowatoa Wamasai kutoka katika ardhi hiyo ambayo ni urithi wa mababu wa jamii hiyo.
Ujumbe aliouandika Rais kupitia ukurasa wake wa Twitter juzi Novemba 23 unasomeka hivi; “…There has never been, nor will there ever be any plan by the Government of #Tanzania to evict the #Maasai people from their ancestral land…“– @jmkikwete

Katika taarifa zilizoenea kwenye vyombo vya habari ilisemekana kuwa lengo la kuiondoa Jamii hiyo ni kuwapatia eneo lenye kilometa za mraba 1,500, kampuni ya OBC ya Falme za Kiarabu.

MOROCCO YAWAKAMATA WAPIGANAJI WA DAESH


Washukiwa sita wametiwa mbaroni nchini Morocco baada ya mkanda wa video kuwaonyesha wanaume sita waliovalia maski wakitangaza utiifu wao kwa kundi la kigaidi la Daesh, linalozusha hofu na wasiwasi huko Iraq na Syria. Watu watatu walitiwa mbaroni jana na wengine watatu hapo jana. Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Morocco imeeleza kuwa, mkuu wa kundi hilo na washirika wenzake wawili walifungwa jela mwaka 2008 nchini humo kwa kuhusika katika njama za ugaidi na kuwa na uhusiano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida.

Vikosi vya usalama na polisi wa Morocco wamenasa pia simu ya mkononi iliyokuwa ikitumiwa na magaidi hao kurekodia picha za video na visu alivyokuwa navyo mmoja wa washukiwa hao. Watu hao sita waliotangaza utiifu wao kwa kundi la kitakfiri la Daesh wametiwa mbaroni baada ya ripoti za vyombo vya habari kueleza kuwa, mkanda ulioonyeshwa wiki iliyopita, ulirekodiwa huko Morocco. Mkanda huo wa video uliwaonyesha wanaume watatu wakiwa na bendera ya Daesh huku wakijiarifisha kuwa wanachama wa kundi hilo la kigaidi.